Wasiomtambua Mungu walaani mwanamke kupigwa kofi
NA PETER MBURU
Muungano wa watu wasitambua uwepo wa Mungu nchini (Atheists In Kenya) umeghadhabishwa na kitendo cha mwanamume kutoka kaunti ya Nyeri kumzaba kofi afisa wa kike wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC), na umeapa kufuatilia suala hilo hadi haki itendeke.
Katika video inayosambaa mitandaoni, mwanamume huyo anayedaiwa kuwa wa kikundi cha mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua anaonekana akimzaba kofi mwanamke huyo, baada ya makibiliano ya maneno kwa muda kuhusiana na uchaguzi mdogo wa wodi ya Ruguru.
Mbunge huyo alifika katika kituo kimoja cha kupigia kura akidai kuwa baadhi ya maafisa wa IEBC walikuwa wafuasi wa mmoja wa wapiganiaji wa kiti cha uwakilishi wa wodi hiyo.
Kufuatia kitendo hicho cha aibu, muungano wa AIK ulighadhabika na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, ambayo pia ilichapishwa kwenye ukurasa wao wa facebook, kulaani kitendo chenyewe.
Kwenye habari hiyo iliyo na jina Daisy Siongok kama naibu wa rais wa muungano wa AIK, wanasisitiza kuwa hawataruhusu haki za wanawake kudhalilishwa.
“Kitendo hicho ni dhuluma ya kijinsia na ni kukiuka haki za binadamu. Ni kitendo cha kupingika na kukatalika katika kila jamii iliyostaarabika,” ikasema habari yao.
“Imejulikana kuwa dhuluma kama hii ya jinsia imejikita katika taasubi zetu za kiume na tamaduni potovu zinazokubali dhuluma dhidi ya wanawake- haswa kutoka kwa wanaume. Hata baada ya kitendo hicho, polisi hawakuchukua hatua mara moja kumkamata mhalifu,” akasema Bi Siongok.
Muungano uliahidi kufuatilia suala hilo hadi mwisho wake, ili kuhakikisha kuwa mwanamke aliyedhulumiwa amepata haki yake.
“AIK inasimama kulaani kila aina ya dhuluma dhidi ya wanawake,” ikamalizia habari yao.
Hii, hata hivyo ilikuwa baada ya mtuhumiwa wa kitendo hicho kukamatwa na kufikishwa kortini.