Habari Mseto

Uhusiano wangu na Chebukati ni mzuri zaidi, masaibu yangu yanatoka nje – Chiloba

April 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA
KWA mara ya kwamza Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) aliyesimamishwa kazi  kwa muda Ezra Chiloba Ijumaa alidai kuwa matatizo yanayoizonga tume hiyo yanachochewa kutoka nje.
Akiongea na wanahabari kwa mara ya kwanza nyumbani kwake Kitale, tangu alipoamriwa kwenda likizo ya lazima ya miezi tatu, Bw Chiloba alisema madai kwamba tuna tofauti zozote kati yake na mwenyekiti Bw Wafula Wanyonyi Chebukati.
“Ukweli ni kwamba uhusiano kati yangu na mwenyekiti ni mzuri zaidi. Matatizo yanayoshuhudiwa katika IEBC yanaletwa na watu fulani kutoka nje,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi.
“Haya mnayoyaona yakifanyika katika tume yanaashiria wazi kuwa utendakazi na shughuli zake zinaingiliwa pakubwa,” akasema Bw Chiloba ambaye alisema wakati huu anajishughulisha na shughuli za kilimo nyumbani kwake Kitale.
Hata hivyo, Bw Chiloba alielezea matumaini kuwa shida zinazoisibu IEBC yatasuluhishwa hivi karibu kumwezesha kurejelea majukumu yake.
Afisa huyo alisimamisha kazi Ijumaa wiki jana ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusu  madai kwamba alipeana zabuni za ununuzi wa vifaa vya uchaguzi bila kufuata taratibu za kisheria.
Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa makamishna watano  wa IEBC chini ya uongozi wa wa Chebukati. Kura ilipopigwa Bw Chebukati, Prof Abdi Guliye na Boya Molu waliunga mkono kusimamishwa kazi kwa Bw Chiloba huku Bi Consolata Maina (Naibu Mwenyekiti) na Dkt Paul Kurgat wakipinga. Bi Margaret Mwachanya alikuwa nje ya nchini kwa ziara rasmi jijini Dubai katika Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE).
Siku mbili baadaye, Bi Maina, Bi Mwachanya na Dkt Kurgat walitangaza kuwa wamejiuzulu kutokana na kile walichotaja na uongozi mbaya wa Bw Chebukati.