• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:45 AM
Seneti kujadili hali ya maambukizi ya corona

Seneti kujadili hali ya maambukizi ya corona

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti Jumanne, Machi 31, 2020, litafanya kikao cha kwanza, majuma mawili baada ya kuahirisha shughuli zake kutokana na tisho la virusi vya corona.

Maseneta watajadili hali ya maambukizi ya ugonjwa huo nchini na hatua ambazo serikali imeweka kuudhibiti kufikia sasa ambapo jumla ya watu 50 wameambukizwa na mmoja kufariki.

Spika Ken Lusaka alisema maseneta watakaohudhuria kikao hicho kitakachoanza saa nane na nusu alasiri watadumisha kanuni ya mmoja kukaa umbali wa angalau mita moja kutoka kwa mwingine.

Kanuni hiyo imependekezwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na inatekelezwa na serikali ya Kenya kupitia Wizara ya Afya.

“Kwa kuwa sheria za bunge la seneti zinaruhusu uwepo wa angalau maseneta 15 kushiriki shughuli ukumbini, mipango imewekwa kuhakikisha kuwa ni maseneta wanachache watafika Jumanne. Tutahakikisha kanuni ya kuepuka mtagusano kama njia ya kuzuia maambukizi ya virusi hivi,” Bw Lusaka akasema wiki jana kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Seneti yarejelea vikao huku kukiwa na hofu kwamba huenda wabunge kadhaa waliotangamana na mwenzao wa Rabai Kamoti Mwamkale wamepata virusi hiyo.

Bw Mwamkale aliambukizwa virusi vya corona baada ya kutangamana na Naibu Gavana wa Kilifi Gedion Saburi aliyeambukizwa virusi hivyo nchini Ujerumani alikozuru mapema mwezi Machi.

Jumla na wabunge 50 na wahudumu kadhaa wa bunge ambao walitangaza na mbunge huyo wanafanyiwa uchunguzi.

Duru zasema kuwa Bunge la Kitaifa litafanya kikao maalum mnamo Jumanne wiki ijayo kujadili na kuidhinisha sheria faafu kuwezesha kutekelezwa kwa mikakati ambayo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuzuia makali ya janga hili kwa uchumi wa Kenya.

Baadhi ya mikakati hiyo ni kupunguzwa kwa ushuru za ziada ya thamani (VAT) kutoka asilimia 16 hadi asilimia 14 na kuondolewa kwa aina zote za ushuru kwa waajiriwa wanaopokea mishahara isiyozidi Sh24,000 kwa mwezi.

You can share this post!

Rais wa zamani wa Congo afariki baada ya kuugua corona

KAFYU: Wanne wanusurika kifo

adminleo