Habari Mseto

KAFYU: Wanne wanusurika kifo

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA SAMMY WAWERU

Watu wanne walinusurika kifo Jumatatu jioni baada ya gari walimokuwa kuhusika katika ajali mbaya katika barabara kuu ya Thika.

Ajali hiyo iliyofanyika eneo la Carwash, kilomita moja kutoka Kasarani, ilihusisha magari matatu, dakika chache kabla ya kafyu kuanza kutekelezwa.

Kulingana na manusura wa gari ndogo la kibinafsi na lililoathirika pakubwa, lori la kusafirisha changarawe, liliendeshwa kwa mwendo wa kasi likibadilisha leni bila uangalifu.

Dereva wa lori hilo alidaiwa kutoroka baada ya kusababisha mkasa, na kurejea maafisa wa trafiki walipowasili.

“Nilianza kushuku lori hili kuanzia Roysambu, kutokana na lilivyoendeshwa bila uangalifu wa magari yaliyo nyuma na mbele,” alilalamika dereva wa gari aina pick-up, ambalo pia lilihusika.

Dereva wa gari ndogo alidai alikuwa katika leni ya kutoka barabara ya kasi, na gari lake lilisukumwa hadi leni ya kasi zaidi. “Tulikuwa tunaelekea Juja, ni Mungu aliyetuokoa,” alisema, akiongezwa kwamba alihisi maumivu kwenye bega la mkono wa kulia.

Madereva wametakiwa kuwa waangalifu wakiwa barabarani, hasa wakati huu taifa limegubikwa na janga la Covid – 19.

“Hatutaruhusu utepetevu wa aina yoyote ile barabarani. Hebu tazama athari za msongamano zilizojiri kufuatia tukio hili, watu wakijaribu kufika makwao kabla ya kafyu kuanza kutekelezwa,” alionya afisa mmoja wa trafiki kutoka kituo cha polisi cha Kasarani, Nairobi.

Mkasa huo ulitatiza shughuli za uchukuzi kwa saa kadhaa, gari lililoharibika kupita kiasi likifutwa dakika chache kabla ya saa mbili za jioni.

Visa vya ajali kushuhudiwa kati ya mtaa wa Githurai na Kasarani, Thika Super Highway si vigeni. Uendeshaji magari kwa mwendo wa kasi na kubadilisha leni bila uangalifu unatajwa kama kiini kikuu cha ajali katika barabara hiyo ya kasi.