Habari Mseto

CORONA: Maisha dijitali kwa makanisa

March 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA SAMMY WAWERU

Wiki moja baada ya serikali kuamuru makanisa yote nchini kusitisha kwa muda usiojulikana waumini kuhudhuria ibada ili kuzuia maenezi zaidi ya Covid – 19 nchini, mengi yamegeukia mitandao ya kijamii kufanya mahubiri.

Mnamo Jumapili, makanisa kadhaa yalitumia mtandao wa Facebook Live, kupeperusha kwa njia ya video mahubiri, yaliyoandamana na nyimbo. Pia, kuna yaliyotumia vyombo vya habari; runinga na redio kufikia washirika na wananchi.

“Baada ya ibada, mchungaji alituma na kuchapisha nambari (Pay Bill) ya kutuma sadaka na fungu la kumi,” Susan Njoroge, ambaye ni mshirka wa Pefa Kimbo, Ruiru akaambia Taifa Leo Dijitali.

Sawa na kanisa hilo, The House of Destiny Church, Kerugoya, pia liliendesha mahubiri yake kupitia mtandao wa Facebook Live. Jackline Kinyua, mshirika, amesema kanisa hilo la Kerugoya linaendesha huduma zake kupitia mtandao huo. “Huduma za kila siku tunazitoa kupitia mitandao, ingawa si zoezi rahisi,” akasema.

Licha ya agizo la serikali, wahubiri na makasisi wachache walionekana kukaidi amri na kukongamana makanisani, japo mkono wa sheria na ambao ni mrefu haukuwasaza.

Kwenye uchunguzi wa Taifa Leo Dijitali katika baadhi ya mitaa Nairobi na Kiambu, makanisa yalisalia na kufuli mlangoni. Kati ya kadhaa tuliyozuru, ni kanisa moja tu, Gospel Restoration Glorious Church, Zimmerman Nairobi, lililofunguliwa.

Aidha, kanisa hilo lilikuwa na washirika wawili, waliocheza piano iliyoandamana na nyimbo. Kanisa moja la dhehebu la Akorino, eneo la Zimmerman, lilitoa ujumbe kwa waumini wake: “Hakuna huduma mpaka wiki mbili zijazo kwa sababu zisizoepukika,” sehemu ya ujumbe huo inaeleza.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alionya kuwa watakaopatikana wakikongamana kwenye makanisa na maeneo mengine ya kuabudu, watachukuliwa hatua kisheria. Mabaa na maeneo ya burudani, pia yalipigwa marufuku ili kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona. Amri ya kutotoka nje kati ya saa moja za jioni na saa kumi na moja asubuhi, kila siku inaendelea kutekelezwa kote nchini.

Kifo cha mgonjwa mmoja wa Covid – 19 kimeripotiwa hapa nchini, jumla ya 50 wakithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo hatari.