CORONA: Kanisa lashangaza kuendea sadaka katika nyumba za washirika
Na STEPHEN MUNYIRI
KUTOKANA na hatua ya serikali kupiga marufuku ibada za Jumapili kote nchini kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona duniani, baadhi ya makanisa yamebuni njia mpya za kukusanya sadaka.
Kanisa moja katika Kaunti ya Nyeri limeanza kukusanya sadaka na fungu la kumi kwa kwenda majumbani mwa washirika wake.
Na kutokana na hatua hiyo, baadhi ya washirika wa kanisa hilo katika wadi ya Ruguru, Kaunti Ndogo ya Mathira Magharibi wameeleza mshangao wao.
Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, walisema kwamba, walishangaa Jumapili iliyopita, wakati mashemasi walifika majumbani mwao na kuwataka kuwapa sadaka zao kama ilivyo kawaida kila Jumapili.
“Nilikuwa najitayarisha kumpeleka mamangu hospitalini, wakati mmoja wa mashemasi alifika nyumbani na kuniambia kwamba amefika kuchukua sadaka. Sikuwa na habari kuwa wangefika. Sikuwa na pesa za kutosha, hivyo nililazimika kutoa fedha chache nilizokuwa nazo ili kuepuka aibu,” akasema mshirika mmoja wa kanisa hilo ambaye hakutaka kutajwa.
Washirika hao walisema kuwa hawapingi mbinu hiyo, lakini hailingani na mafundisho ya Biblia, kwani kiwango cha fedha ambazo mtu alitoa kilinakiliwa katika kitabu. Walieleza kuwa huo ni ukiukaji wa mafundisho hayo, kwani pesa ambazo mtu anatoa kama sadaka ama fungu la kumi zinapaswa kuwa siri.
“Biblia inaeleza kuhusu umuhimu wa faida za kuchanga. Tunapaswa kutoa michango kulingana na uwezo wetu kifedha. Hilo linamaanisha kwamba mtu anaweza kutoa mchango mkubwa kuliko fungu la kumi na wakati mwingine uwe mdogo. Yote yanalingana na uwezo wa kifedha wa mshirika husika,” akasema mshirika mwingine wa kanisa hilo.
Mwingine alinukuu kitabu cha Wakorintho wa Pili 9:7 kinachosema: “Mungu anapenda anayetoa mchango kwa kujitolea kwa moyo wake wote; wakati tunapotoa kwa mioyo michangamfu, bila kujali ikiwa fedha hizo zitatumika kama sadaka ama kumsaidia mtu aliye katika shida, ni kitendo cha kumfurahisha Mungu.”
Mtu mwingine alieleza: “Makanisa mbalimbali yana mbinu tofauti za kukusanya sadaka. Mara nyingi, utoaji sadaka huandamana na nyimbo, maombi ama yote mawili.
“Baadhi ya madhehebu huwa yanakusanya sadaka katikati ya ibada, huku mengine yakikusanya mwishoni mwa ibada zao. Hakuna utaratibu maalum uliotajwa kwenye Biblia kuhusu vile sadaka na michango inapaswa kukusanywa. Hivyo, makanisa yako huru kutumia njia zozote.”
Katika Kaunti ya Tharaka-Nithi, baadhi ya washirika walisema kuwa kanisa lao liliwapa nambari maalum ambayo wangetumia kutuma michango yao.