• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Gavana Mandago apiga marufuku wazee kuingia mijini

Gavana Mandago apiga marufuku wazee kuingia mijini

TITUS OMINDE na SAMUEL BAYA

GAVANA wa Uasin Gishu, Jackson Mandago amepiga marufuku wazee kuzuru sehemu za miji katika kaunti hiyo hadi janga la corona liangamizwe.

Alisema hatua hiyo haipaswi kuchukuliwa kama ubaguzi dhidi ya wazee, bali inalenga kuwalinda vilivyo dhidi ya virusi hivyo.

Bw Mandago aliwataka wazee wa umri wa miaka 60 na zaidi watumie wadogo wao kutafuta huduma mjini humo.

“Tunaheshimu na kuthamini wazee wetu. Ndio sababu tumetoa amri kwa wazee wa miaka zaidi ya 60 kukaa nyumbani bila kutembelea mji huu hadi pale ugonjwa huu utakapokabiliwa,” alisema Bw Mandago.

Alikuwa akirejelea takwimu za kutoka nchini Italia ambapo idadi kubwa ya watu ambao walifariki kutokana na virusi hivyo ni wazee.

Hata hivyo, msimamo wake ulipingwa na Mzee Jackson Kibor ambaye ameoa binti wa miaka 36.

Kwingineko, shule za mabweni zitakazotumika kama vituo vya kuwashughulikia wagonjwa wa Corona katika ukanda wa Bonde la Ufa zitajulikana wiki hii.

Msimamizi wa eneo hilo Bw George Natembeya anasema, shughuli ya kuzikagua shule hizo inaendeshwa na maafisa kutoka idara ya elimu na wale wa afya.

“Maafisa wangu kutoka kwa idara ya elimu ya afya wamekuwa wakiangalia shule za malazi ambazo ziko na miundo msingi ambayo inaweza kutumika kama maeneo ya kuwahudumia wagonjwa wa virusi vya Corona. Kwa sasa wanaandaa ripoti hiyo na wataitoa wiki hii. Baada ya ripoti hiyo, sasa wakazi watajua ni wapi ambapo watakuwa wanaweza kupeleka wale ambao wanaugua,” akasema Bw Natembeya.

Hata hivyo, alisema kuwa licha ya serikali kujitahidi kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanywa kuzuia kuendelea kusambaa kwa virusi vya Corona, ni wakenya wenyewe ambao watahakikisha wako salama kwa kufuatilia yale masharti ambayo serikali inataka yafuatwe.

“Hata tukiweka hivi vituo vya kupeleka waathiriwa wa virusi hivyo, sio serikali ambayo itaenda huko. Serikali haiwezi kupata virusi. Ni wewe Mkenya ambaye hufuati masharti ndiwe utakayeenda kulala katika maeneo hayo peke yako. Kwa hivyo Wakenya wanafaa kusikiliza kwa makini na kufuata yale masharti yote ambayo tunaweka kwa sababu haya yote ni kwa ajili ya usalama wao,” akasema afisa huyo.

Kadhalika, Bw Natembeya alisikitishwa na idadi kubwa ya wakazi wa Bonde la Ufa ambao hawataki kuzingatia mikakati ambayo iliwekwa na wizara ya Afya ikukoa maisha.

You can share this post!

Wakazi wa Korogocho wanufaika na mitungi ya maji na vieuzi

KICD na Safaricom kufunzia watoto nyumbani

adminleo