• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
WATOTO: Anatumia umahiri wake katika usakataji densi kuikosoa jamii

WATOTO: Anatumia umahiri wake katika usakataji densi kuikosoa jamii

Na PATRICK KILAVUKA

MASIHA ya kidijitali yana manufaa na athari zake kwa jamii.  Ni kutokana na kauli kwamba uzingativu wa usasa na kizazi kipya unaathiri jamii moja kwa moja, ambapo mwanadensi Hilda Njoki,14, mwanafunzi wa darasa la nane shule ya msingi ya Iveche, Kaunti ya Embu aliongoza wengine kupitia wasilisho la densi ya kisasa.

Lengo lake lilikuwa kupitisha ujumbe mahsusi kuhusu vile mitandao ya kijamii inatia makovu kwa jamii kupitia maadili potovu na ambayo yananogwa kwenye mitandao hiyo baada ya wao kuzama katika uraibu wa kuitizama au kuitumia.

Hilda Njoki (kulia) aungana na wenzake kusakata densi ya kisasa. Picha/ Patrick Kilavuka

Hasa mada kuu ilikuwa kuhamasisha watoto wa kizazi kipya kumakinika katika masomo kuliko kutizama vipindi vya runinga ambavyo huwapotosha kimaadili.

Njoki aliongoza wanadensi wenzake kuwasilisha ujumbe huo katika mashindano ya kitaifa ya Maigizo na Filamu ambayo yaliandaliwa shule ya Upili ya Lenena, Nairobi na wakaibuka magwiji wa densi ya kisasa.

Anawaongoza wenzake kunengua viuno. Picha/ Patrick Kilavuka

Njoki akiongoza kikundi hiki cha wasakataji densi, waliwasilisha densi yenye dibaji ya The Walking Call ambayo ilikuwa inagusia uraibu wa mwanafunzi moja aliyekuwa amezama katika kutumia wakati wake mwingi katika masuala ya mitandao ya kijamii hususa televisheni na kusahau kuwianisha na masomo kisha akafeli mtihani.

Lakini alijielewa baadaye kisha akatia bidii masomoni baada ya kuasi uraibu huo na akaimarisha kiwango cha masomo kisha akafua dafu katika mtihani. Kwa upande mwingine, kulikuwa na dada yake aliyegubia mabuku kwa kujitolea na akapita mtihani.

Njoki aibuka mcheza densi bora wa kike na kutuzwa. Picha/ Patrick Kilavuka.

Densi hiyo ilikuwa bora katika kategoria ya Densi ya Kisasa kwa kuwa na maudhui bora bunifu, uelekezi bora, uelekezi bora wa ishara na ya pili ya ubora wa jezi na ulimbwende.

Mwelekezi Alex Gitonga alituzwa mwelekezi bora wa konyezo ilhali tuzo la mwekelezi bora lilimwendea mwalimu mkuu Joyce Njamwo. Kombe la mwanadensi bora wa kiume lilimwendea Prince Brian Murithi wa shule hiyo.

Hatimaye, shule ilituzwa vikombe vitano na vyeti baada ya kutawazwa bingwa wa densi hiyo.

Wasakataji bora, akiwemo Njoki, wapokea vyeti kwa bidii yao. Picha/ Patrick Kilavuka

Njoki aliyepokea cheti cha msakataji bora wa kike, alianza kuwa nahodha wa kikundi tokea walipoanza kushirki katika mashindano ya kaunti ndogo ambayo yalifanyiwa shule ya Embu Special na kuwawezesha kutoa nafasi ya kwanza kisha kupata tiketi ya kushirki katika mashindano ya Kaunti yaliyoandaliwa shule ya upili ya Kangaru na kuwa wa kwanza kukata utepe wa mashindano na kusonga mbele kwa ya Kanda.

Mapambano ya Kanda ya Mashariki yalifanyiwa shule ya Wasichana ya Kaaga na wakawa kileleni tena.

Hatimaye, kampeni ya kuwakilisha kanda na shule chini ya uongozi wake ilifika kilele katika kinganyanyiro cha kitaifa na kuonesha ueledi wa kusakata densi ya kisasa na kutawazwa bingwa wa kitaifa kategoria hiyo.

Njoki ashindana na mwanadensi bora wa kiume Prince Brian Murithi. Picha/ Patrick Kilavuka

Hata hivyo, katika mashindano ya viwango vitatu tangulizi (Kaunti ndogo hadi Kanda), alitawazwa kuwa mwanadada wa kike mahiri katika kusakata densi ya kisasa na kupokea vyeti pia.

Kando na kushiriki katika mashindano ya kitaifa, mwanadensi chipukizi huyo amekiongoza kikosi kushirki katika Mkutano wa Walimu Wakuu Wasimamizi wa Shule za Mashariki ambao uliandaliwa Kawa, Embu  na wakapokea vyeti vya kushirki.

Yeye ni kiongozi pia wa kikundi cha kunengua cha The Shakers  Dancers shuleni na kile cha Sakata Dancers.

Manufaa ya usakataji? Anasema densi imemfikisha mbali, kutagusana na watu mashuhuri , kumakinika kimasomo kwani ni zoezi tosha kwa afya bora na humweka kisaikolojia fiti. Fauka ya hayo, amechochea talanta ambayo yaweza kuwa ajira siku za usoni.

Njoki afanya mazoezi na mwalimu wake. Picha/ Patrick Kilavuka

Angependa kuwashukuru wazazi na dadaye Linda Nyakio kwa kumtia motisha. Isitoshe, mwalimu mkuu , walimu na wanafunzi wenzake kumtia moyo kukuza kipawa chake.

Uraibu wake ni kucheza handiboli, kusakata densi ya kitamaduni na kuimba.

Ushauri kwa wasanii ni kwamba, watilie maanani kile wangependa kufanya maishani na wataona ndoto zao zikitmia.

Pia, wasikate tamaa au kushushwa moyo na wakinzani kwa sababu maisha ni safari yenye changamoto za kukabiliwa kwa kujiamini na kile unaweza.

You can share this post!

Hatimaye Moi aifariji familia ya Matiba

Wagonjwa wanafariki tukitazama, serikali iwajibike –...

adminleo