• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Sonko hatimaye alisha Meja Jenerali pilipili ya siasa za jiji

Sonko hatimaye alisha Meja Jenerali pilipili ya siasa za jiji

Na COLLINS OMULO

WIKI tatu baada ya kuanza kazi, Mkurugenzi wa Nairobi Metropolitan Services (NMS), Mohamed Badi ameanza kutofautiana na Gavana Mike Sonko na chama cha wafanyakazi wa serikali ya kaunti ya Nairobi.

Vita vinatokota kati ya mkurugenzi huyo na Gavana Sonko anayeungwa mkono na chama cha wafanyakazi wanaokataa kuhamishiwa NMS.

Mnamo Ijumaa, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ilihamisha wafanyakazi 6,052 wa serikali ya kaunti ya Nairobi hadi NMS kuanzia wiki hii.

Tume iliwaeleza kuwa, watakuwa chini ya afisi hiyo mpya na sio bodi ya huduma ya umma ya kaunti ya Nairobi.

Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua mwezi jana aliwateua maafisa 32 wa vyeo vya juu, hatua ambayo iliacha mawaziri wa kaunti, maafisa wakuu na wakurugenzi katika njia panda

Ni maamuzi haya ambayo yamechemsha Bw Sonko na viongozi wa chama cha wafanyakazi ambao wako tayari kumkabili Bw Badi.

Gavana Sonko alikuwa wa kwanza kulaumu hatua hiyo kwa kuwataka wafanyakazi wa kaunti kupuuza barua ya uhamisho na vitisho vya PSC akiwaambia kuwa bodi ya uajiri ya kaunti itawashauri kuhusu mfumo wa uhamisho utakaotilia maanani maslahi yao.

“Wafanyakazi wote wa serikali ya kaunti ya Nairobi wanaagizwa kupuuza mawasiliano yoyote kuhusu kuhamishwa kwa majukumu kutoka kwa yeyote ikiwa mawasiliano hayo hayako kwa maandishi na kunakiliwa kwa gavana na karani wa kaunti,” Sonko alisema.

Alilaumu NMS na PSC akisema hazina mamlaka ya kutoa maagizo ya aina yoyote kwa wafanyakazi wa kaunti ya Nairobi.

Alisisitiza kuwa, kuhamishwa kwa baadhi ya majukumu hadi serikali kuu hakumaanishi serikali ya kaunti ilivunjwa na akalaumu baadhi ya maafisa wakuu serikalini kwa kukiuka sheria na mkataba wake na serikali ya kitaifa wakilenga kutimiza maslahi yao ya kibinafsi.

NMS ilikua imeagiza karibu wafanyakazi 600 wa kaunti wakongamane leo katika jumba la KICC kwa maagizo zaidi, lakini Jumamosi Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema mkusanyiko huo ni kinyume na maagizo ya serikali kuhusu juhudi za kukabili maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

WANDERI: Yawezekana tunaishi nyakati za mwisho?

Wazee wataka mitishamba itumike kutibu corona

adminleo