Habari Mseto

Msaada kwa wakazi wa Westlands

April 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

Kampuni ya Myspace Properties imejitosa katika kupunguzia mzigo familia zisizojiweza maarufu kama chokoraa wakati huu mgumu wa janga la virusi vya corona kwa kupatia familia hizo kutoka eneobunge la Westlands blanketi, barakoa na vyakula.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi, Myspace, ambayo ilipatia familia hizo blanketi 100 na pia mikate na maziwa miongoni mwa vyakula vingine, imesema kuwa familia 100 zilinufaika na msaada huo wake, ambao imeongeza kuwa ni kionjo tu.

“Tangu kisa cha kwanza cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kithibitishwe nchini Kenya (mnamo Machi 13), maisha hayajakuwa kawaida kwa kila mtu bila ya kujali tabaka ya mtu katika jamii. Kila mtu anaishi kwa hofu. Mambo yamekuwa magumu hata zaidi kutoka kafyu ianze (Machi 27) kwa sababu sasa maisha ya karibu kila mwananchi yameathirika.

“Hata hivyo, wanaoumia zaidi ni familia zisizo na makao na zile za wasiojiweza (chokoraa),” taarifa hiyo ilisema, huku kampuni hiyo ikifichua kuwa iliguswa sana na video ya chokoraa iliosambaa kwenye mitandao ya kijamii wakiomba wahisani kuwapa blanketi, vyakula, barakoa na vitu vingine muhimu vitakavyowasaidia wakati huu mgumu.

Baadhi ya chokoraa hao walisema ni raia wa Sudan Kusini na Burundi, wengi wao waliotoroka nchi zao kwa sababu ya hali ngumu katika mataifa yao.

“Tunatoa kile tunacho si kwa sababu sisi tuko na mali nyingi, lakini kwa sababu ya moyo wa kujitolea na kuonyesha upendo kati yetu…tunajua kuwa watu walioumia sana wakati huu mgumu wa virusi vya corona na kafyu ni familia za chokoraa ambazo hazina vyakula wala nyumba. Baada ya kuona video hiyo, tuliamua kuzisaidia. Tunaomba wahisani wengine wasimame na familia hizi wakati huu mgumu.

“Kila mwananchi ana jukumu la kukabiliana na virusi vya corona. Itakuwa upumbavu tukiangalia tu kwa hofu kutoka mbali, kuangalia upande mwingine kana kwamba hatuoni kinachoendelea ama kutochangia kadri tunavyoweza na kutarajia serikali itatufanyia kila kitu.

“Huu ndio wakati wa kukuja pamoja na kukabliana na adui huyu anayeitwa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo,” Afisa Mkuu Mtendaji Mwenda Thuranira alisema.