• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Corona yakata gharama kali ya mazishi nchini

Corona yakata gharama kali ya mazishi nchini

Na BENSON MATHEKA

GHARAMA ya kuandaa mazishi nchini imepungua pakubwa tangu serikali ilipoagiza miili kuzikwa saa 24 baada ya kifo kutokea katika juhudi za kupunguza maambukizi ya virusi vya corona.

Katika muda wa wiki tatu sasa, mazishi yamekuwa yakihudhuriwa na watu wachache wa familia kufuatia agizo la serikali ya watu kutokusanyika kwa shughuli za umma.

Agizo hili la serikali limepunguzia familia nyingi gharama ya mazishi iliyotokana na miili kuhifadhiwa mochari kwa muda mrefu huku mochari za kibinafsi zikiathiriwa kwa kukosa wateja.

Watu wengi hasa maeneo ya mashambani wameamua kutopeleka miili mochari na badala yake wamekuwa wakiizika mara moja, hatua ambayo imepunguza gharama ya mazishi.

“Shughuli katika mochari yetu zimepungua kwa sababu idadi ya miili inayoletwa kuhifadhiwa imepungua pia. Hata wanaoileta wanaichukua baada ya siku moja kwenda kuizika tofauti na awali ambapo miili ilikuwa ikichukua wiki moja hivi watu wakiandaa mazishi,” asema afisa mmoja wa mochari ya Monalisa and Montezuma ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu si msemaji wa kampuni hiyo.

Mochari hiyo hutoza Sh1,000 kwa siku kuhifadhi mwili na Sh7,000 kwa muda wa wiki moja. Familia nyingi zilikuwa zikifanya harambee kugharimia mazishi.

“Hatua ya serikali imepunguza gharama ya mazishi kwa kiwango kikubwa kwa sababu hata wageni wamepungua, tofauti na awali ambapo watu walikuwa wakifanya harambee kulisha waombolezaji. Siku hizi ni watu 15 pekee ambao wanahudhuria mazishi na huwa wanatawanyika baada ya kuteremsha mwili kaburini,” asema katibu wa chama cha Kalunga Funeral Welfare Association katika Kaunti ya Machakos, Joseph Kimotho.

Anasema hii ni afueni kwa familia nyingi kwa kuwa hakuna gharama ya kuchapisha vijitabu kuelezea maisha ya marehemu, kuajiri watu wa kupiga picha na video na hafla za kitamaduni zilizokuwa zikigharimu maelfu ya pesa.

“Kwetu kama chama, mzigo umepungua. Tunachoshughulika ni gharama ya kununua jeneza marehemu akifariki akiwa nyumbani na kusafirisha maiti ya wanaofariki wakiwa mbali na nyumbani,” asema.

Kwa watu wanaopoteza wapendwa wao wakiwa maeneo ya mijini, gharama wanayoshughulikia ni ya kusafirisha maiti maeneo ya mashambani ambako inazikwa na watu wachache wa familia?Kabla ya agizo la serikali waliofiwa walikuwa wakisaidiwa na marafiki kukusanya pesa za kugharimia mazishi ya wapendwa wao.

Kila jioni, kulikuwa na mikutano katika mikahawa na kumbi mbalimbali mijini kutayarisha mazishi. Kaunti kadhaa ziliagiza mochari zote kufungwa wakati huu wa kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Hii ilitokana na agizo la serikali kwamba miili yote izikwe saa 24 baada ya kifo kutokea na kuhudhuriwa na watu wasiozidi 15.

Hata hivyo, agizo la serikali limeathiri familia maskini katika maeneo ya mashambani zinazopoteza wapendwa wao wakiwa mbali na nyumbani.?Baadhi yao walikuwa wakitegemea wahisani kupata pesa za kulipa bili za hospitali, mochari na kusafirisha maiti za wapendwa wao kwa mazishi maeneo ya mashambani. Maafisa wa utawala wa mikoa wameagizwa kuhakikisha agizo la serikali limetekelezwa kikamilifu.

You can share this post!

Kenya Power yakaidi waziri na kukatia kampuni ya maji umeme

Mikakati hii si ya kuwatesa, ni ya kuwalinda – Rais...

adminleo