Habari Mseto

Mikakati hii si ya kuwatesa, ni ya kuwalinda – Rais Kenyatta

April 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Rais Uhuru Kenyatta ametetea vikali mikakati aliyotoa jana inayodhibiti shughuli za usafiri na uchukuzi kaunti zinazotajwa kuathirika zaidi na Covid – 19.

Kiongozi wa nchi, kwenye hotuba yake kwa taifa katika Ikulu ya Rais, aliagiza safari za kuingia na kutoka kaunti ya Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale, kusitishwa kwa muda wa siku 21. Amri hiyo pia inahusisha sehemu kadhaa kaunti ya Kiambu.

Usafiri na shughuli za biashara ndani ya kaunti hizo zitaendelea kama kawaida.

Katika kaunti ya Nairobi, amri hiyo ilianza kutekelezwa jana jioni, huku Mombasa, Kilifi na Kwale ikitarajia kuanza kutekeleza kesho.

Mapema Jumanne, kwenye mahojiano ya pamoja na yaliyoshirikisha vituo vitatu vya redio, Kameme Fm, Coro Fm na Inooro Fm, vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Agikuyu, Rais Kenyatta alisema agizo hilo halitaathiri wenye sababu za kimsingi na zinazoeleweka, kama vile wanaotoka mbali kuenda kutafuta matibabu jijini Nairobi.

“Mikakati tuliyoweka si ya kutesa watu ni ya kuwasaidia,” Rais akasema. Kufuatia kafyu inayoendelea kutekelezwa kote nchini kati ya saa moja za jioni hadi saa kumi na moja za asubuhi kila siku, baadhi ya maafisa wa polisi wanaoshika doria wamenyooshewa kidole cha lawama kwa kuhangaisha raia, Bw Kenyatta akiwataka kuitekeleza kwa njia ya utu.

“Nimeambia askari wetu na wanaoshika doria wasihangaishe watu. Ikiwa ni mgonjwa ametoka Nyeri, au sehemu yoyote ile nchini, mruhusu aingie, mmepeleke katika hospitali ahudumiwe kisha umrejeshe,” Rais akahimiza, katika mahojiano hayo yaliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya Nairobi.

Rais alisema wanaofungiwa kuingia na kutoka kaunti zilizotajwa, ni wanaoenda “kujivinjari”, katika mchakato mzima kusaidia kudhibiti maambukizi zaidi ya Covid – 19. Magari ya mizigo, hasa vyakula na dawa yanaruhusiwa kuingia na kutoka, ingawa pia yamewekewa mikakati maalum.

Kulingana na idara ya afya, kaunti ya Nairobi ndiyo inaongoza kwa maambukizi ya virusi hivyo hatari vya corona. Rais ameendelea kuhimiza Wakenya kufuata maagizo na utaratibu uliotolewa na wizara ya afya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na zaidi ya visa 150 vya wagonjwa wa Covid – 19, sita wakifariki kutokana na virusi hivyo.