CORONA: Waiguru aponea kung'atuliwa mamlakani
Maureen Kakah na George Munene
GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga, Jumanne alipata afueni baada ya mahakama kusimamisha kwa muda kujadiliwa kwa hoja ya kumwondoa mamlakani.
Jaji Weldon Korir wa Mahakama Kuu aliagiza kuwa bunge la kaunti hiyo linapaswa kusitisha mpango huo hadi janga la corona litakapodhibitiwa nchini.
Kwenye agizo hilo, jaji huyo alisema kuwa kujadiliwa kwa hoja hiyo kwa sasa kutakuwa sawa na kuingilia haki za kisiasa za Bi Waiguru.
“Kwa maoni yangu, hali ilivyo inahitaji mahakama kuingilia kati mpango wa bunge, hasa wakati huu nchi inapokabili virusi vya corona. Mpango huo unatishia haki zake na hitaji la ushirikiano wa taasisi za serikali kuyakabili majanga,” ikaagiza mahakama.
Bi Waiguru alisema anatekeleza agizo la Serikali ya Kitaifa kwa maafisa wake kufanyia kazi kutoka majumbani mwao.
Jaji Korir alisema kwamba utaratibu huo unamhitaji gavana na wakili wake kuwepo kwenye bunge.
Vile vile, mahakama ilisema kuwa ushirikishi wa wananchi kwenye hoja hiyo utaathiriwa na kanuni zinazowazuia watu kukongamana katika maeneo ya umma.
“Sioni sababu yoyote maalum kwenye madai kwamba hoja hiyo inapaswa kusimamishwa kwani haijazingatia taratibu zifaazo za sheria. Hata hivyo, suala la virusi vya corona ni lenye uzito na linapaswa kuchukuliwa kwa makini,” akasema Jaji Korir.
Jaji alitoa uamuzi huo kwenye kesi ambapo Bi Waiguru alilishtaki bunge hilo na Spika wake Jumanne iliyopita ili kusimamisha mpango wa kumwondoa mamlakani.
Bunge linamlaumu gavana kwa madai ya ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka na kutoishirikisha kwenye masuala muhimu yanayohusu uongozi wa kaunti.