Habari Mseto

Wasafiri wataabika kukwama mpakani

April 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

WASAFIRI kutoka Thika kuelekea Murang’ a walikwama katika mpaka wa kaunti hizo mbili.

Magari ya usafiri na ya kibinafsi yalizuiliwa na polisi yalipofika eneo la Blue Post ambapo ni mpaka wa kaunti ya Kiambu na Murang’ a.

Juhudi za wasafiri hao kujitetea kuwa hawakufahamu agizo la rais yalikosa kusikizwa na walinda usalama ambao walikuwa wakizuia magari yasipite upande wa pili.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Gatanga Bw Paul Karobia, alisema walipata maagizo maalum kuwa hakuna gari yoyote ambayo iliruhusiwa kupita hadi upande wa pili kutokana na maagizo hayo yaliyotolewa na serikali

“Wananchi wengi bado hawataki kufuata maagizo kamili waliyopewa kwani hata baada ya kuombwa washuke kutoka kwenye magari bado walizidi kubishana na walinda usalama,” alisema Bw Karobia.

Alisema wengi wao walilazimika kutembea miguu baada ya kushuka kutoka kwa Matatu.

“Hatutawaruhusu wananchi kutembea hata kwa miguu kuvuka upande wa pili Wa kaunti jirani kwa sababu hiyo ni njia moja ya kujumuika pamoja,” alisema Bw Karobia.

Amewahimiza wananchi kufuata maagizo ya serikali ili tuweze kukabiliana na janga hili la Corona.

“Sasa sio wakati wa mabishano bali ni kushirikiana pamoja na kufuata maagizo yote yaliyowekwa na serikali,” alisema afisa huyo wa usalama.

Mnamo Jumatatu rais Uhuru Kenyatta alitoa maagizo na kusema ya kwamba hakuna ruhusa ya kutoka nje ya kaunti ya Nairibi, Mombasa, Kilifi, na Kwale na pia kuingia.

Hata hivyo magari ya kusafirisha chakula yamekubaliwa kusafiri huku dereva pekee yake akikubaliwa kusafiri.

Hatua hiyo imevuruga kabisa mipango ya watu wengi ambao walikuwa wamesafiri katika kaunti zingine wakitarajia kurejea jijini Nairobi lakini sasa mipango hiyo haipo.