Habari Mseto

Joho kuwapa wakazi wa Mombasa chakula na maji

April 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA
 
USAMBAZAJI wa chakula dawa na maji, bila malipo, kwa wakazi masikini  na wenye mahitaji maalum ni baadhi ya hatua ambazo Gavana  Ali Hassan Joho atachukua kukabiliana na makali ya marufuku iliyoanza kutekelezwa Jumatano.
 
Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, Joho alisema serikali yake imetenga kitita cha Sh200 milioni kufadhili mpango huo.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara mabwanyenye kutoka kaunti hiyo pia wameahidi kutoa Sh100 miliioni kupiga jeki mpango huo ambao utaanza kutekelezwa leo usiku.
Kando na hayo mkuu huyo wa kaunti ya Mombasa alisema kaunti yake inaendelea kutumia Sh324 milioni kununua dawa na vifaa vya matibabu kwa hospitali za umma ili kuwasaidia wananchini wakati huu mgumu.
“Tuko tayari kufanya chochote tuwezalo ili kuhakikisha kuwa watu wetu haswa wale ambao ni wenye mahitaji maalum wanapata mahitaji yao ya kimsingi wakati huu wa kafya na marufuku ya kutoingia na kutotoka Mombasa itakapoanza kutekelezwa,” Bw Joho akasema.
“Hata ikilazimu kwamba tusalimishe asilimia 100 ya mishahara yetu kwa mpango huu, tuko tayari kufanya hivyo,” akaongeza.
Bw Joho alisema serikali yake imewatambia zaidi ya familia 200,000 zenye mahitaji maalum ambazo zitasambaziwa misaada ya chakula, dawa na maji chini ya mpango huo.
“Kuanzia Jumatano, maafisa wa serikali yangu watakuwa wakizunguza katika makazi ya watu hawa na kuwapa mahitaji ya kimsingi, Tutafanya hii kwa ushirikiano na washirika wetu” akaeleza.
 
“Leo tumegundua kuwa ni watu wetu watashughulikiwa kwanza. Mengine, baadaye. Ikiwa watu wanaendelea kufariki sio haja ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” akaongeza.
Bw Joho alitoa hakikisho hilo saa chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza amri ya kuzuia watu kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Kilifi, Kwale na Mombasa ambazo zimeorodheshwa kama zile ambazo zimeathirika zaidi ya janga la Covid-19.
Amri hiyo ilianza kutekelezwa Nairobi kuanzia Jumatatu saa moja za usiku kwa siku 21.  Na itaanza kutekelezwa Jumatano katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale kwa muda huo huo.