Makahaba walilia msaada wakiahidi kubadilika
Na Titus Ominde
MAKAHABA mjini Eldoret wanawasihi wahisani kuwasaidia kifedha wakiahidi kurekebisha tabia baada ya biashara yao kuathiriwa na janga la corona.
Walisema hawana wateja kutokana na kafyu ambayo imezuia wateja wao kutoka nyumbani usiku.
“Maisha yamekuwa magumu, inaonekana hizi ni siku za mwisho ambazo Biblia inazungumzia. Niko tayari kurekebisha ikiwa nitapata msaada wa kuanzisha biashara mbadala,” alisema Irene Wanjiru (sio jina lake halisi).
Katika mahojiano ya kipekee, Wanjiru alisema ameshindwa kutunza watoto wake watatu kwani kwa wiki mbili zilizopita hajawahi hudumia mteja yeyote.
Alisema tangu kufungwa kwa kumbi za burudani kama vile baa na vilabu vya usiku kwa sababu ya kafyu kutokana na virusi vya corona wateja wao wamesalia nyumbani.
Idadi kubwa ya makahaba ambao walizungumza na Taifa Leo walisema wanajua biashara zao ni haramu lakini wamelazimishwa kushiriki biashara hiyo kwa sababu ya ukosefu wa ajira.
“Nina mafunzo katika taaluma ya hoteli na utalii lakini tangu nifuzu yapata miaka 10 iliyopita sijapata kazi yoyote,” akaongeza
Lakini chama cha makahaba waliorekebisha tabia kiliwaambia wale wanaotaka kubadili tabia zao kikweli waunde kikundi ili kupata msaada kutoka kwa wafadhili.
“Baadhi ya makahaba hawa ni waongo na hawako tayari kurekebisha tabia. Juhudi zetu za kutaka wabadilike ili wanaufaike na msaada kutoka kwa wahisani zimekuwa zikigonga mwamba kwani wengi wao wamekataa kwa kuzoea pesa za bwerere,” alisema Bw Joseph Wanyonyi ambaye kutoka chama hicho.