Habari Mseto

Mateso ya Wakenya China: Serikali yawasilisha barua ya malalamishi

April 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AGGREY MUTAMBO

Kenya imewasilisha malalamishi kwa serikali ya China kuhusiana na picha zilizopeperushwa kwenye ruinga na mitandaoni zikiwaonyesha Wakenya wakilala barabarani baada ya kufurushwa kutoka makazi yao wakishukiwa kuwa na virusi vya corona.

Ilidaiwa kuwa serikali ya China ilichukua hatua hiyo baada kubainika kuwa visa vipya vya maambukizi ya corona nchini humo vilikuwa vikigunduliwa kutoka kwa wageni, haswa wa asili ya Afrika.

Hii ndio maana katika barua yake, Kenya ilisema inafahamu kuwa China inatekeleza kanuni mpya za kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, ikiwemo kuwachunguza watu kwa wingi.

Kwa hivyo, Kenya inatambua kuwa China inalenga “kuzuia kuingizwa kwa visa vya Covid-19 ndani ya mkoa wa Guangzhou na maeneo mengineyo.”

Hata hivyo, Serikali ya Kenya inalalama kuwa baadhi ya hatua hizo “zimechangia baadhi ya raia wa China, haswa wamiliki wa nyumbani, kuwadhulumu wageni, haswa wa asili ya Afrika,”

Katika taarifa, Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Kenya ilisema baadhi ya kuwasilishwa kwa barua yake ya malalamishi kwa ubalozi wa China, Nairobi, serikali ya China imetoa hakikisho kuwa iknafuatilia suala hilo.

“Watawala mkoani Guangzhou wametakiwa kuchukua hatua za haraka za kulinda haki za Waafrika walioathirika,” afisi ya ubalozi wa China, jijini Nairobi ikasema.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni imewataka Wakenya wote nchini China kuwasiliana na

“Ubalozi wetu jijini Beijing iko tayari kushughulikia changamoto zozote ambazo zinaweza kuibuka. Utafanya hivyo kwa kushirikiano na utawala wa Chine”, wizara ikasema.

Ikaongeza, “Kwa kuzingatia kujitolea na ushirikano kati ya mataifa haya mawili, tunatarajia kuwa suala hili litatatuliwa haraka kwa manufaa ya Wakenya walioko China.”

Hata hivyo, Wakenya walioko nchini China wameitaka serikali ya Kenya kuwasaidia warejee nyumbani baadhi ya kushamiri kwa ubaguzi wa rangi dhidhi ya Waafrika baada ya taifa hilo kupata afueni kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Wengi wao wamefurushwa kutoka nyumba zao na sasa wanaishi barabarani huku wengine wakitegemea wahisani kwa mahitaji kama chakula

Iliripotiwa kuwa polisi waliwafurusha kwa nguvu na kutwaa stakabadhi zao

Wakenya wengi wameisuta serikali ya China kwa kufumbia macho dhuluma zinazotendewa Waafrika wasio na hatia huku wakitaka mataifa mengine kupinga unyama huo.

Mkurupuko wa virusi vya corona uliripotiwa kwa mara ya kwanza jijini Wuhan, China mnamo Desemba 31, 2019. Na kufikia sasa taifa hilo limerikodi maambukizi 81,907 na vifo 3,336 kulingana na takwimu rasmi zilizotolewa na serikali ya nchini hiyo.

Hata hivyo virusi hivyo vimesambaa kwa kasi zaidi katika kote ulimwenguni haswa Amerika na Uropa ambapo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu.

Tafsiri: Charles Wasonga