• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
‘Msiwakate mshahara wafanyakazi wa Tottenham’

‘Msiwakate mshahara wafanyakazi wa Tottenham’

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha mashabiki wa Tottenham Hotspur (THST) kinaamini kwamba “bado kuna muda” kwa usimamizi “kufanya maamuzi yanayostahili” baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kupunguza mishahara ya baadhi ya wafanyakazi wake.

Mwishoni mwa Machi 2020, Tottenham walitangaza kwamba wafanyakazi wao 550 ambao si wachezaji wangekatwa asilimia 20 ya mishahara yao kutokana na mlipuko wa virusi vya homa kali ya corona.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti Daniel Levy, Tottenham waliichukua hatua hiyo kwa nia ya “kuhifadhi ajira za wafanyakazi wao wote” katika kipindi hiki kigumu cha kifedha.

Ingawa hivyo, THST imewataka vinara wa kikosi hicho kubatilisha maamuzi hayo kwa kusisitiza kwamba “Tottenham ni kikosi kikubwa” kinachojivunia hazina ya inayowatosha kudumisha mahitaji ya kifedha ya wachezaji na wafanyakazi wake kwa kipindi kirefu.

“Tumefichua msimamo wetu kwa nia safi na tupo radhi kushirikiana na usimamizi wa klabu hiyo katika hali zote kwa minajili ya mafanikio ya kila mshikadau. Tunahisi kwamba bado kuna muda wa kutosha kwa Bodi ya Usimamizi kufanya maamuzi mwafaka yatakayoonyesha kwamba inajali maslahi ya kila mmojawapo wa wafanyakazi wa Tottenham,” ikasema sehemu ya taarifa ya THST.

Levy ambaye alitia mfukoni kima cha Sh980 milioni mwaka jana (Sh560 milioni za mshahara na Sh420 milioni za marupurupu ya kukamilika kwa uwanja wa Tottenham Hotspur), ni miongoni mwa waajiriwa wasiokuwa wachezaji wa Tottenham wakaoathiriwa na hatua ya kupunguziwa mshahara kuanzia mwishoni mwa Aprili 2020.

Tottenham wanamilikiwa na bilionea Joe Lewis kupitia kampuni ya Tavistock, Uingereza. Kwa mujibu wa Jarida la Times Rich nchini Uingereza, utajiri wa Lewis, 83, ulikisiwa kuwa wa Sh61 bilioni kufikia mwisho wa Disemba 2019.

Newcastle United, Bournemouth na Norwich City ni miongoni mwa klabu nyinginezo za EPL ambazo zimepunguza mishahara ya wafanyakazi wao wasiokuwa wachezaji.

Ingawa Liverpool pia walikuwa wamefanya maamuzi hayo hapo awali, hatua hiyo ilikashifiwa pakubwa na baadhi ya mashabiki na tukio hilo likawashinikiza wasimamizi kubadili msimamo.

Kati ya waliokashifu vikali hatua hiyo ya Liverpool ni wachezaji wa zamani wa kikosi hicho, Jamie Carragher na Stan Collymore.

“Liverpool na kocha Jurgen Klopp walikuwa na huruma sana kwa waathiriwa wa corona janga hili la kimataifa lilipoanza. Baadhi ya wachezaji wao wa haiba kubwa walikuwa radhi hata kupunguziwa mishahara yao. Ni ajabu kwamba mambo kwa sasa ni kinyume. Heshima na nia safi iliyokuwapo awali sasa imeyeyuka ghafla,” akasema Caragher katika kauli iliyoungwa mkono na Collymore.

“Sidhani kuna shabiki yeyote timamu wa Liverpool ambaye hatakasirishwa na hatua hii. Maamuzi haya ya kupunguza malipo ya vibarua mara nyingi hufanywa na wafanyabiashara wadogo. Liverpool ni klabu inayomilikiwa na mabwanyenye. Isitoshe, klabu ilipokezwa fedha nyingi sana baada ya kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana na ubingwa wa Kombe la Dunia mwishoni mwa mwaka uliopita,” akaongeza Collymore.

Baada ya juhudi za Liverpool kugonga ukuta, nahodha wao Jordan, ametoa wito kwa klabu, mashirika na wachezaji maarufu wanaopokea mishahara minono katika fani mbalimbali za spoti kuchangia sehemu ya mabilioni yao kupiga jeki vita vya kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona.

You can share this post!

Mfano wa kuigwa

Mashindano ya viziwi yaahirishwa

adminleo