• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Waliotengwa katika hoteli kujilipia bili

Waliotengwa katika hoteli kujilipia bili

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI imejitenga na malipo ya ada za watu walioamua kuishi hotelini walipotengwa ili wasitangamane na jamii kama njia ya kuepusha uwezekano wa kueneza virusi vya corona.

Serikali imewataka watu waliotengwa kwa lazima, hasa walioamua kuishi katika hoteli ya PrideInn Lantana jijini Nairobi katika kipindi hicho cha kutengwa, wagharimie malipo ya muda wote ambao walikaa hotelini humo.

Alhamisi, hoteli hiyo ilisitisha huduma baada ya watu hao walioongezewa muda wa kutengwa kukataa kulipa bili zao na kuitaka serikali kulipa.

Lakini Jumamosi jioni, msemaji wa serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna, alisema kwamba serikali haitawajibikia bili za watu binafsi.

“Walipojichagulia wenyewe kutengwa katika vituo vya kibinafsi, ilikuwa sawa na kuweka mkataba wa kibinafsi na hoteli hizo. Kwa hivyo, watu walio katika hoteli hizi, hasa PrideInn Lantana, lazima walipe bili walizotumia wakikaa katika hoteli hizo,” Bw Oguna alisema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Aliongeza, “Serikali haiwezi kuwajibika kwa bili ambazo zilitokana na uamuzi wa mtu au watu binafsi.”

Waliotengwa katika hoteli za kibinafsi walidai wanahitajika kulipa Sh9,000 kwa siku, ambayo ni sawa na Sh126,000 kwa siku 14.

Bw Oguna alisema kabla ya mpango wa kutenga watu waliowasili nchini kutoka ng’ambo kuanza, walitakiwa kuchagua kati ya vituo vya serikali na hoteli za kibinafsi na kwamba kila mtu alifanya chaguo kutegemea uwezo wake wa kifedha.

“Watu waliochagua vituo vya serikali vya kutenga walioshukiwa kuwa na corona walipelekwa katika vituo hivyo hali wale waliochagua hoteli kama zile zinazomilikiwa na kampuni ya PrideInn zinazoshirikisha Lantana, Azzure na Raphta walipelekwa katika vituo hivyo,” alieleza Bw Oguna.

Alisema mpango wa lazima wa kuwatenga watu hao ulipangiwa kudumu kwa siku 14 kabla ya watu wote katika vituo hivyo kupimwa virusi vya corona.

Endapo kuna yeyote aliyepatikana na corona, muda wa siku nyingine 14 uliongezwa katika kituo husika.

“Vituo ambavyo watu walipatikana na virusi hivyo, wengine katika kituo husika walilazimika kutengwa kwa siku 14 zaidi kwa gharama yao wenyewe. Watu hao walikuwa na chaguo la kuhamia vituo vya serikali au kubaki katika hoteli za kibinafsi,” alisema Bw Oguna.

Kulingana naye, kutengwa kwa watu hao kwa muda zaidi kulifaa ili kulinda jamii kutokana na virusi vya corona.

“Katika hoteli ya PrideInn Lantana watu waliotengwa huko walikataa kufuata masharti ya kutengwa na kusababisha baadhi yao kuambukizwa virusi vya corona na kwa hivyo ikabidi watengwe kwa siku 14 zaidi,” alisema.

Mnamo Ijumaa Wizara ya Afya ilisema kuwa imeanza kufunga vituo ambavyo waliotengewa humo walidumisha nidhamu na kufuata maagizo.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alisema katika baadhi ya vituo waliotengwa walikuwa wakiandaa karamu na kukaribiana, hatua iliyoongeza hatari ya kusambaza virusi vya corona.

Idadi kubwa ya watu 197 walioambukizwa virusi hivyo nchini ni wale waliokuwa katika vituo hivyo.

You can share this post!

Aliyekufa kwa corona azikwa bila utaratibu

Sonko agutuka alijivua mamlaka akabaki uchi

adminleo