Safari ya Moi ikuluni yawa telezi Ruto akizidi kutia kibindoni wafuasi

Na CHARLES WASONGA

HARAKATI za Seneta wa Baringo, Gideon Moi za kutaka kutwaa wadhifa wa kigogo wa siasa katika jamii ya Kalenjin baada ya kifo cha babake, marehemu Daniel Moi, zinakumbwa na mawimbi makali ya kisiasa.

Wadadisi wanasema mawimbi hayo ya kisiasa yaliyoshuhudiwa katika ngome hiyo mwezi jana, yanaonekana kumfaidi mshindani wake mkuu katika ubabe wa siasa za janibu za Wakalenjin, Naibu Rais William Ruto.

Kwanza, Diwani ya Kanu anayewakilisha Wadi ya Churo/Amaya, Ameja Zelemoi alitimuliwa kutoka wadhifa wa Naibu Spika wa Bunge la Kaunti ya Baringo. Pili, katika mwezi huo huo, mamia ya wakazi wa mji wa Kabarnet walifanya maandamano katika barabara za mji huo wakilaani kile walichokitaja kama kutengwa na kubaguliwa kwa Dkt Ruto serikalini. Maandamano sawa na hayo yalifanyika mjini Eldoret.

Maandamana hayo yalijiri siku moja baada ya Mbunge Mwakilishi wa Kina Mama Baringo, Gladwell Cheruiyot Tungo, kusoma taarifa iliyoandaliwa na wabunge wa mrengo wa Kieleweke ambako walimshinikiza Dkt Ruto ajiuzulu baada ya afisi yake kuhusishwa na sakata ya utoaji zabuni feki ya ununuzi wa silaha.

Mhusika mkuu katika sakata hiyo ya Sh39 bilioni ni aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa, mwandani wa Dkt Ruto.

Tatu, tangu Januari mwaka huu, wanasiasa kutoka jamii ya Kalenjin ambao ni waasi wa Naibu Ruto wamesitisha shutuma dhidi yake huku mwandani wa Seneta Moi, Alex Tolgos (Gavana wa Elgeyo Marakwet) akifutilia mbali mipango ya kuandaa mkutano wa BBI mjini Eldoret kwa hofu ya kuvurugwa na wafuasi Dkt Ruto.

Miongoni mwa wabunge waliokimwa hata kabla ya janga la virusi vya corona kuzima mirindimo ya kisiasa nchini ni; Silas Tiren (Moiben), Alfred Keter (Nandi Hills) na Joshua Kandie (Baringo ya Kati). Mwingine ni aliyekuwa mwaniaji ugavana wa Uasin Gishu katika uchaguzi mkuu wa 2017, Zedekiah Bundotich.

Wabunge waasi wa Dkt Ruto ambao walieendelea kumpigia debe Gideon na kumshutumu Naibu huyo wa Rais ni William Kamket (Tiaty) na Joshua Kuttuny (Cherangany).

Philip Chebunet, ambaye ni mchanganuzi wa siasa kutoka eneo la North Rift, juzi alinukuliwa akisema kuwa, matukio hayo ya kisiasa ni pigo kubwa kwa Gideon ambaye wakati wa mazishi ya babake alipokezwa “rungu la nyayo” kama ishara ya mamlaka.

“Kushindwa kwa mwenyekiti huyo wa Kanu kuwashawishi madiwani wa Bunge la Kaunti ya Baringo wasimwondoe mamlakani Diwani Zelemoi kutoka wadhifa wa Naibu Spika, kuliashiria kwamba, ameshindwa kudhibiti siasa za kaunti hii ambako amechaguliwa mara mbili kama Seneta,” akasema.

Dkt Chebunet akaongeza: “Ikiwa hali ni hivyo Baringo, basi Gideon angali na kibarua kikubwa kujiimarisha kisiasa katika kaunti zingine, kama vile Nandi, Uasin Gishu, Kericho, Bomet, Elgeyo Marakwet na Trans Nzoa ambako kuna idadi kubwa ya watu wa jamii ya Kalenjin.

Wakati wa hafla ya mazishi ya Mzee Moi, mnamo Februari mwaka huu, Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat alitangaza kuwa, Gideon angeanza kampeni ya kukivumisha kote nchini kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022. Mwanasiasa huyo alisema shughuli hiyo itaendeshwa baada ya “chama chetu kumwomboleza Mzee kwa kipindi cha siku 40.”

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU), Francis Atwoli, ambaye alimtaka Seneta huyo wa Baringo kurejesha sifa na ushawishi ambao chama hicho kilikuwa nayo chini ya uongozi wa marehemu babake.

Hii ndio maana mnamo Machi 4, Seneta Moi alihudhuria mkutano wa BBI katika uwanja wa Kinoru, Meru na kutoa matamshi yaliyoashiria kuwa chama chake kinapania kubuni muungano na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Wakati huu wajibu wetu mkubwa ni kumsaidia Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza ajenda zake za maendeleo kwa Wakenya. Lakini wakati ukitimu, tutashirikiana na vyama vyenye maono sawa na yetu, kuwapa Wakenya uongozi bora,” akasema.

Na siku chache baadaye, Seneta Moi alipokea jumbe za wanasiasa kutoka kaunti za Siaya na eneo la Mlima Kenya nyumbani kwa babake, Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Lakini ujumbe wa wanasiasa kutoka Mlima Kenya uliovutia hisia za kisiasa kwani ulisheheni wanasiasa watajika kama vile Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu na Seneta wa Nyeri Ephraim Maina.

Bw Waititu, al maarufu, Baba Yao alitangaza kuwa amehama Jubilee na kujiunga na Kanu huku akichukua fursa hiyo kumwalika Seneta huyo wa Baringo azuru eneo la Mlima Kenyatta avumishe Kanu.

Bw Martin Andati anasema Seneta Moi alipasa kualika jumbe za viongozi wanasiasa kutoka kaunti za jamii ya Kalenjin kwanza kabla ya kupanua mtandao wake kwa kaunti zingine.

“Wema huanza nyumbani. Baada ya kifo cha babake ambaye alihusudiwa zaidi katika janibu za Kalenjin, kibarua cha kwanza kwa Gideonkingekuwa kujiimarisha katika kaunti zote za jamii hiyo, kuanzia Baringo,” anasema Andati.

Habari zinazohusiana na hii

KONDOO WA RUTO MATAANI