Habari Mseto

Fundi aonyesha ubunifu wake katika uundaji wa barakoa za watoto

April 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JAMES MURIMI

FUNDI wa nguo katika mji wa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, ameanza kutengeneza barakoa maalumu za watoto, baada ya kugundua kwamba nyingi zilizopo zimetengenezewa watu wazima pekee.

Hili linalenga kuimarisha mikakati ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona. Bw Peter Wainaina alianza kutengeneza maski hizo zilizo na mitindo ya kuvutia watoto, baada ya kuacha kushona mavazi ya wanawake na wanaume.

Anaendesha hilo kupitia Mpango wa Uvumbuzi na Maendeleo wa Kaunti ya Laikipia.

Bw Maina ni mojawapo wa wamiliki cherehani wengine wanane kutoka kaunti hiyo, ambao walipewa mafunzo maalum katika Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi, Nyeri, kuhusu utaratibu wa kutengeneza vifaa vya kuwasaidia wananchi kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

“Niliamua kuanza kutengeneza barakoa hizi baada ya kubaini kuwa watoto ni kama wamesahaulika kwenye juhudi za kukabili maambukizi ya virusi hivyo. Niligundua kuwa wazazi wengi wanatembea katika maeneo mbalimbali wakiwa wamezivalia, huku watoto wao wakiwa hawajavalishwa kifaa chochote ili kuwalinda,” akasema jana kwenye mahojiano na Taifa Leo kwenye duka lake.

Akiwa na wenzake 20 walio chini yake, anatarajia kutengeneza maski zaidi za watoto na watu wazima kutokana na uhitaji wake mkubwa.

“Nimetengeneza maski hizi kwa muundo ambao utawavutia watoto kuzivaa mara nyingi. Tunatengeneza muundo wa wanyama, ambao unahitaji ubunifu wa hali ya juu. Ninauza kila maski Sh100 kwani zinaweza kuoshwa na kuvaliwa tena,” akasema Bw Maina.

Alieleza kuwa maski hizo zinaweza kuvaliwa kwa kila upande, lakini zina uwezo wa kuzuia viini kuingia kwa yule aliyevalia. Vilevile, zinawaruhusu watoto kupumua kwa urahisi.

Duka la Bw Maina sasa limekuwa lenye shughuli nyingi, kwani mamia ya wazazi wanafika ili kununua maski zao na za watoto wao.

“Nimenunua maski mbili za mume wangu na zingine mbili za mwanangu. Mwanangu anapenda simba, ndipo nimeamua kununua barakoa yenye muundo huo. Haitamsumbua kwa vyovyote vile hata akienda kucheza na watoto wengine,” akasema Bi Jane Wanjiku. Mshonaji huyo huwa anauza maski za kawaida kwa Sh20. Kabla ya kuanza kuzitengeneza, huwa anaweka dawa maalum kwa kitambaa ambacho hutumiwa kuzishona.

Alieleza aliamua kutengeneza maski ambazo zinaweza kutumiwa zaidi ya mara moja, alipogundua kwamba wakazi wengi hawakuwa wakimudu kununua zile zinazotumika mara moja.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetaja uvaaji maski katika maeneo ya umma kama mojawapo ya njia za kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.