• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Walibora alinikuza kifasihi – Mwandishi wa Taifa Leo Wanderi Kamau

Walibora alinikuza kifasihi – Mwandishi wa Taifa Leo Wanderi Kamau

Na WANDERI KAMAU

PROFESA Ken Walibora ni mwandishi aliyekuwa kwenye kiwango chake maalum cha uandishi.

Alikuwa na upekee wake; upekee ambao hauna waandishi wengi hadi sasa. Aliifahamu vyema hadhira yake.

Nilianza kuchambua rasmi kazi zake marehemu mnamo 2016, baada ya uzinduzi wa jarida la ‘Lugha na Elimu’ kwenye gazeti la ‘Taifa Leo.’

Jarida hilo lina kitengo maalum kiitwacho ‘Mapitio ya Tungo’ ambacho huangazia kazi mbalimbali za waandishi kama riwaya, tamthilia, tawasifu, wasifu na diwani za mashairi na hadithi fupi.

Tangu wakati huo, nimesoma na kupitia kazi nyingi sana za Prof Walibora, baadhi zikiwa ‘Mbaya Wetu’, ‘Ndoto ya Amerika,’ ‘Naskia Sauti ya Mama’, ‘Nimeshindwa Tena’, ‘Upinde Mwingine,’ ‘Ndoto ya Almasi’, ‘Damu Nyeusi’ kati ya nyingine.

Upekee mkubwa wa ukumbi huo ni kwamba umenipa nafasi  kugatusana na waandishi wengi, hasa kuhusu mawazo yao.

Utofauti wa kazi na utunzi wa Prof Walibora umejitokeza kwenye masuala mengi; baadhi yakiwa kiwango cha lugha, mtiririko wa vitushi, ujenzi wa maudhui na wahusika kati ya mengine.

Kuhusu kiwango cha lugha, ilikuwa dhahiri kwangu, kama msomaji mwingine kujifunza msamiati mpya. Hili ni kupitia maneno, tanakali, methali na misemo ya Kiswahili.

Ni nadra sana kusoma kazi ya Prof Walibora ambayo haina sehemu ya ‘Sherehe’; ambayo hutoa nafasi kwa msomaji kujifunza misamiati mipya ya Kiswahili.

Hili limedhihirika kutoka riwaya ya ‘Siku Njema’ aliyochapisha mnamo 1996.

Vile vile, hakuwa anatumia Kiswahili cha kawaida tu, bali alijaribu pakubwa kuleta misemo ya lugha kama Kiarabu, lakini yenye ukuruba mkubwa na matumizi ya Kiswahili cha wastani.

Baadhi ya misemo aliyozoea kutumia kwenye kazi zake ni ‘maddal basari’ kumaanisha kubwa sana, ‘ahlan wa sahalan’ kumaanisha ‘vivi hivi tu’ kati ya mingine mingi.

Kijumla, kazi zake zilikuwa za kufurahisha na kumuelimisha kila aliyezichangamkia.

Utofauti mwingine uliodhihirika kwenye kazi za Prof Walibora, ni uwezo wake mkubwa katika kubuni mtiririko wa vitushi.

Kwa mfano, kumbukumbu kuu ya wengi kuhusu riwaya ‘Siku Njema’ imechangiwa pakubwa na mtiririko wa vitushi, na jinsi mwandishi aliweza kuwajenga wahusika na kuwaoanisha na mazingira walimokuwa.

Hilo ndilo lililozifanya kazi zake nyingi kuwavutia wasomaji wengi katika kila kiwango.

Uwezo huo ndio ulimfanya kuandika kazi ambazo zinatumika katika kila kiwango cha elimu.

Kwa mfano, wakati riwaya kama ‘Kufa Kuzikana’ inaweza kuwekwa katika kiwango cha shule za upili, vyuo anuwai na vyuo vikuu, baadhi ya kazi zake kama ‘Nimeshindwa Tena’ zinanawafaa sana wasomi wa kiwango cha shule za msingi.

Hivyo, ni mwandishi aliyeibeba na kuijukumia jamii kwa nafsi yake yote.

Kimaudhui, Prof Walibora alikuwa mwandishi aliyekita jicho lake la uandishi katika kila uwanda unaoihusu jamii. Alikuwa mwenye mwonolimwengu mpana sana.

Aliangazia siasa, mapenzi, elimu, mazingira, athari za ukabila, madhara ya utawala mbaya kati ya mengine mengi.

Ni mwandishi aliyeamini kuwa ukamilifu wa jamii haupo katika uwanda mmoja tu; bali ni kila nyanja inayohusu maisha ya kila siku.

Kwa mfano, riwaya ‘Kidagaa Kimemwozea’ ni usawiri kamili wa jinsi mfumo wa utawala umedorora barani Afrika kutokana na mgawanyiko wa kitabaka.

Kwenye riwaya hiyo, anawafananisha wananchi na “vidagaa” (samaki wadogo) ambao wananyanyaswa na samaki wakubwa (yaani watawala).

Anazamia masuala mengi riwayani, kwa kuonyesha jinsi nchi nyingi zilivyokosa kutimiza malengo yake ya uhuru baada ya kutekwa na viongozi wafisadi na wanaopenda nafsi zao tu.

Uandishi wake pia haukuishia kwenye riwaya tu, mbali pia aliandika tamthilia kadhaa, baadhi zikiwemo ‘Ahsante ya Punda’ na ‘Mbaya Wetu.’

Baada ya kuanzishwa kwa safu ya ‘Mapitio ya Tungo’ mnamo 2016, nilikuwa miongoni kwa watu kwa kwanza kuichambua tamthilia ‘Mbaya Wetu’ majuma machache ilipozinduliwa.

Nilipoanza kuisoma, iliniteka. Sikuiweka chini kwa siku mbili. Sababu? Mtindo ule ule wa Profesa.

Ingawa tamthilia hiyo inajikita kwenye masuala yenye uzito mkubwa, kuhusu tabia ya wananchi kuwachagua viongozi wabaya kwa kisingizio cha “kuwa wao”, ameiandika kwa mtindo wa kicheshi unaoeleweka na msomaji wa kiwango chochote.

Alizindua tamthilia wakati Kenya ikijitayarisha kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa 2017. Hivyo, ilionekana kama “onyo” kwa wananchi kutathmini pakubwa aina ya viongozi wanaowachagua.

Alitumia tamthilia hiyo kukemea sana maovu kama ufisadi, ambao umekuwa kama saratani isiyoisha katika nchi nyingi za Afrika.

Mhusika mkuu riwayani ni Mburumatari Hatari Bin Temba, anayetumika kama mfano wa jinsi viongozi wapotovu wanavyowapotosha wananchi kuwachagua licha ya kuwa wenye doa kuu.

Bila shaka, wengi ambao wamesoma kwa uketo kazi za Prof Walibora, wamegundua kwamba ameathiriwa sana na mfumo wa uandishi wa Shaaban Bin Robert.

Hili ni kwa kuwajenga na kuwatakasa wahusika na mazingira waliyoishi.

Mfano mkuu ni mhusika Msanifu Kombo (Kongowea Mswahili) kwenye riwaya ‘Siku Njema’ au Imani na Amani kwenye riwaya ‘Kidagaa Kimemwozea.’

Hii ni mbinu ambayo waandishi wengi hawajafaulu kuitumia ili kujengea kazi zao kuishinikiza jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili.

Prof Walibora pia amekiri kuathiriwa pakubwa na waandishi Ngugi wa Thiong’o, Gakaara Wanjau na William Shakespeare.

Ingawa kuna orodha kubwa ya waandishi aliosoma kazi zao, alikiri kwamba hao ni miongoni mwa waliomwathiri sana.

Prof Ngugi, kwa mfano, ndiye aliyemshawishi kuandika tawasifu ‘Nasikia Sauti ya Mama’, ambapo alitarajia pia kuandika mwendelezo wake ikiwa Mwenyezi Mungu angeendelea kumweka hai.

Alisema alishawishika kuandika riwaya hizo baada ya kusoma tawasifu za Ngugi, ambazo ni ‘In The House of Interpreter’ na ‘Dreams in a Time of War.’

Vile vile, alikubali kushawishika kuandika tawasifu hiyo kwa kutangamana na mwandishi Adam Shafi, aliyeandika tawasifu yake iitwayo ‘Mbali na Nyumbani.’

Cha kushangaza ni kwamba, Prof katumia mbinu na usimulizi wa kifasihi kuelezea hadithi kuhusu maisha yake.

Hivyo, tawasifu yenyewe ina usimulizi wa kiriwaya, hivyo kumchangamsha na kumwerevusha msomaji.

Hapana shaka yoyote kwamba,  Prof Walibora ni miongoni mwa waandishi watakaoishi kukumbukwa daima katika fasihi ya Kiswahili kutokana na mchango usio mfano.

Wengi walimpa msimbo wa ‘Shakespeare wa Kiswahili’ kutokana na mchango wake katika kuikuza lugha hiyo.

Kando na Prof Said Ahmed Mohamed, kutoka Tanzania, ambaye yungali hai, hakuna mwandishi aliyefikisha idadi ya vitabu alivyoviandika Ken.

Na si idadi tu, bali vitabu vyenye uzito wa kimawazo na utunzi.

Binafsi, nimepoteza rafiki wa karibu, ambaye alikuwa tayari kuchukua simu zangu kila wakati nilimtafuta kunipa mwongozo na ushauri kuhusu Kiswahili.

Nilizungumza naye mara ya mwisho mnamo Januari 9, nikitafuta kauli yake kuhusu kifo cha mwandishi na msomi, Prof Euphrase Kezilahabi,  kutoka Tanzania. Bado nina arafa niliyomtumia.

Ametutanguliza mbele ya haki. Na ingawa ametuacha, kazi zake zitaweka kumbukumbu yake kwa vizazi na vizazi vijavyo.

Mola amlaze pema peponi. Amin!

 

Taifa Leo Dijitali wiki hii itakuwa ikichapisha taarifa za wapenzi wa Kiswahili waliotangamana na nguli wa lugha Prof Ken Walibora, aliyefariki Ijumaa wiki iliyopita. 

You can share this post!

Yasikitisha Walibora hataona diwani yangu aliyoifasiri...

Wahubiri waomba makanisa yafunguliwe kwa zamu

adminleo