Je, ni kweli barakoa za kushonewa mtaani zinazuia maambukizi ya corona?
Na GEOFFREY ANENE
HUKU biashara ya kushona na kuuza barakoa zilizotengenezwa kwa kutumia vitambaa ikinoga kote nchini Kenya, mjadala umezuka kuhusu uwezo wa barakoa za aina hiyo kuzuia maambukizi ya virusi hatari vya corona.
Aina tatu za barakoa zimekuwa zikizungumziwa sana kwenye mitandao ya kijamii, huku ile ya N95 ikiaminika kuwa bora kabisa kwa sababu inaweza kuzuia maambukizi ya virusi hivyo kwa asilimia 95.
Inafuatiwa na barakoa za kufanyia upasuaji, ambazo pia zina uwezo wa asilimia 95 wa kuzuia virusi kupenyeza, lakini haziwezi kuzuia bakteria, vumbi na poleni kwa asilimia 100 kama N95.
Madai ni kuwa barakoa za kushona kwa kutumia nguo hazina uwezo wa kuzuia maambukizi.
Mwandishi huyu alitafuta ukweli wa habari hizo kutoka kwa madaktari watatu wanaohudumu hapa jijini Nairobi na kuthibitisha kuwa kuvalia barakoa za vitambaa ni afadhali kuliko kuwa bure.
“Barakoa za kushonwa kwa kutumia vitambaa zinapitisha vitone. Hata hivyo, kuwa na barakoa hii ni bora kuliko kukosa kuvalia barakoa. Ndio hazizuii vitone, lakini ni porojo kuwa asilimia yake ya kuzuia maambukizi ni sifuri. Hakuna mtu amefanya utafiti kuthibitisha kuwa uwezo wake ni asilimia sifuri. Hata hivyo, zinasaidia katika kufumba polisi macho ili ukiivalia usikamatwe na kushtakiwa ama kupigwa faini,” alisema daktari Magada, ambaye anajihusisha na matibabu ya mgonjwa ya kuambukizana.
Dkt Tom Mboya anasema virusi vya corona vinasambazwa kupitia vitone kwenye hewa. “Vinaenezwa mtu anapokohoa ama kupiga chafya na pia mtu anayepata vitone hivyo kuvuta pumzi hiyo ama kugusa macho yake ama kinywa. Kwa jumla, barakoa inazuia mtu aliyeivalia kuangukiwa na vitone hivyo, lakini pia inazuia mtu ambaye ni mgonjwa kueneza virusi hivyo,” anasema Mboya na kukubaliana na Magada kuwa kuvalia barakoa yoyote ni bora kuliko kukosa kuvalia barakoa.
“Barakoa za aina ya N95 na upasuaji ndizo nzuri kabisa, lakini zinafaa kutengewa wahudumu wa afya pekee kwa sababu ziko chache kote ulimwenguni na pia wako katika hatari zaidi ya kuambukizwa wanapohudumia wagonjwa. Barakoa za kutumia vitambaa hazina uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya virusi, lakini ni nzuri katika kuzuia vitone kuanguka ovyo na kwa hivyo zinazuia nafasi ya kuambukiza watu karibu nasi,” anasema.
Kuhusu barakoa za kutengenezwa kwa kutumia vitambaa, daktari Fredrick Okong’o anasema lazima ziwe zimeshonwa kwa kutumia vitambaa vitatu. Amesifu barakoa za kushonwa akisema, “ni rahisi kuoshwa.”
Aidha, Magada ameonya Wakenya dhidi ya kuvua na kuvaa barakoa kila mara bila ya kusafisha mikono yao. “Tunafanya kazi bure tukivaa barakoa halafu kila mara mtu anaivua na kuivaa bila ya kusafisha mikono. Inafaa ukivua barakoa, safisha mikono yako kwanza kabla ya kuivaa tena,” alisema.
Naye Mboya ameshauri, “Mataifa ambayo yamefaulu kupunguza visa vya maambukizi yamefuata maagizo inavyotakikana. Naomba sisi sote tufuate maagizo ya kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji, kusafisha mikono kwa kutumia ‘sanitaiza’ na kuvalia barakoa tunapokuwa kwenye umma. Kumbuka kukaa mbali na watu wengine kila wakati.”
Okong’o pia ametaka Wakenya wote wavalie barakoa “kwa sababu huwezi kujua nani ana virusi vya corona na nani hana.” “Hakikisha barakoa yako ni safi kabla ya kuivalia kila asubuhi. Iweke kwenye kemikali ya kuua viini vya maradhi usiku mzima,” anashauri.