Habari Mseto

Walibora hakujua kuficha uozo, alieleza yaliokuwa moyoni bila kutetereka – Kennedy Wandera

April 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

NA KENNEDY WANDERA

Nilikutana na Prof Ken Walibora Juni 22, 2016 saa 8:02 katika makao makuu ya taasisi yaukuzaji mitaala nchini Kenya KICD jijini Nairobi katika juhudi za kupanua na kueneza matumiziya lugha ya Kiswahili ukanda wa Afrika Mashariki.

Hapa palikuwapo wataalamu na wanahabari wa Kiswahili. Hapa lengo lilikuwa moja tu: Kuzindua rasmi Chama cha Wanahabari wa Kiswahili Mashariki mwa Afrika-CHAWAKIMA.

Mwanzoni, madhumuni yalikuwa ni kuanzisha Chama cha Wanahabari wa Kiswahili nchini Kenya-CHAWAKIMA-KENYA kama tawi mojawapo la chama kikuu CHAWAKIMA.

Wadau wa lugha waliohudhuria uasisi wa chama hiki walikuwa ni pamoja na Profesa Kenneth Inyani Simala, Katibu Mtendaji, Kamisheni ya Kiswahili maarufu kama East Africa Swahili Commission, Profesa Ken Walibora, Mwanahabari, Shirika la Habari la Nation, Charles Otunga, Mwanahabari, Shirika la Habari la KBC, Ramadhan Kibuga, Mwanahabari, Shirika la Habari la BBC kutoka Burundi, Henry Indindi, Mtaalam wa Kiswahili, Jacob Riziki kutoka Burundi nami nikiwa Mwanahabari wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, VOA.

Dondoo za uzinduzi zilinakiwa na Bw Otunga na hapo kwenye kikao tukamteua Prof. Walibora kuwa Mwenyekiti nami naibu wake, Jacob Riziki aliteuliwa kuwa katibu kuendeleza mikakati yakubuni chama cha wanahabari nchini Burundi-CHAWAKIMA-BURUNDI.

Mkutano huu ulifanyika baada ya kukamilika warsha ya siku mbili ya Baraza la Kiswahjili la Afrika mashariki lililozungumzuia kwa mapana swala zima la ustawishaji wa lugha ya Kiswahili na nafasi yake kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo hususan katika taasisi za elimu namaisha ya wadau wa lugha hiyo.

Katika kikao hiki kilichoongozwa na Prof. Simala, wanachama tulitakiwa, tukifuata itifaki yaJumuiya ya Afrika Mashariki ya kuhamasisha umuhimu wa kubuniwa vyama vitakavyokuzalugha ya Kiswahili, Prof Walibora alisisitizia umuhimu na jukumu la vyombo vya habari katikamchakato wa kukuza lugha ya Kiswahili kupitia mawanda mengine ya lugha, utafiti nauoanishaji wa mitaala na usanifishaji wa lugha katika nchi za Afrika Mashariki yaani Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Katika mahojiano niliofanya naye ambayo yanapatikana hapa: http://www.voaswahili.com/a/3368248.html kuanzia dakika ya 22:16-26:25.

Prof. Walibora anaeleza hivi, “Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa. Tunafikiria kuwa mustakabali wa Kiswahili ni mzuri sana lakini vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kukisaidia kukieneza Kiswahili. Na kuundwa chama hiki ambacho sisi tunakiita CHAWAKIMA kitasaidia kusanifisha istilahi na msamiati unaotumika katika vyombo vya habari ili wasikilizaji wasitatanike sana.”

Kutokana na juhudi hizo za Prof Walibora, chama hicho kipo hai kikiwa na wakilishi kutoka Zanzibar, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi. CHAWAKIMA-KENYA kimekuwa chini ya uongozi wake akiwa Msemaji wa chama.

Viongozi wengine wa chama hiki ni Mathias Momanyi, Mwanahabari na Mzalishaji wa vipindi KBC akiwa Mwenyekiti, Bw Otunga ni Mlezi wa chama, Victor Wetende ambaye ni mkurugenzi wa Mawasiliano katika serikali ya jimbo la Vihiga ni Katibu nami nikiwaKatibu Mwenezi huku Doreen Gatwiri akiwa Mwekahazina.

Prof. Walibora hakuwa tu msomi kama wasomi wengine. Alisimama kidete na kazi za Kiswahili. Alifurahia wote waliokieneza kwa nguvu zao zote.

Nikimhoji Februari 23, 2017 kufuatia kifo cha mtunzi stadi wamashairi Sheikh Ahmed Mohamed Nabhany, Matondoni, Lamu nchini Kenya, Prof. Walibora alitumia maneno yote mazuri kumuomboleza Nabhany akimtaja kuwa mtu wa kupigiwa mfano katika uundajiwa misamiati na istilahi za lugha ya Kiswahili.

Si wengi wanaopongeza tungo za wengine. Walibora hakuwa na kiwi, hakuwa na kinyongo. Alishabikia uwezo wa wandishi chipukizi na kwa wale walioonekana kujigamba na kujishabikia kuwa viranja wa lugha aliwakumbusha, “Kiswahili ni nyumba moja tusigombanie ufito”

Oktoba 5, 2017 inasalia kwenye kumbukumbu, siku hii nilimtafuta Prof. Walibora kufahamu hisia zake kuhusu Tuzo ya fasihi ya Nobel inayotolewa na Taasisi ya Taaluma ya Uswidi kuhusu Lugha na Fasihi aliyopokezwa Kazuo Ishighuro,62, raia wa Uingereza.

Msomi maarufu na mwandishi wa ‘Weep Not Child’, ‘A Grain of Wheat’ na ‘The River Between’ Professa Ngugi wa Thiong’o kwa mara ya pili alikuwa ameipoteza. Prof. Ngugi Wa Thiong’o tangu mwaka wa 2010 amekuwa akipigiwa upatu kushinda tuzo hii lakini bado hajabahatika.

Profesa Walibora alionekana kutoshtuka na maamuzi ya jopo la Taasisi ya Taaluma ya Uswidi, ‘Mimi sioni la ajabu wala sishangazwi na jopo linaloteua washindi wa tuzo ya Fasihi ya Nobel kutompa kwa mara nyingine Mkenya Ngugi wa Thiong’o. La msingi ni kwamba siku zote hata anapopigiwa upatu kwamba atashinda mimi huwa na shaka kwa sababu ya masuala ambayo labda hayaambatani moja kwa moja na ubora wa vitabu alivyoviandika au mchango wake katika uandishi wa fasihi barani Afrika au duniani kote hapana. La msingi ni kwamba tuzo ya fasihi ya Nobel hutolewa kwa mwandishi ambaye anaandika yale ambayo lile jopo linataka.”

Profesa Walibora hakujua kuficha uozo. Alieleza yaliokuwa moyoni bila kutetereka. Nimesema naye mwisho mwezi wa Machi mwaka huu kumhoji kupata ufafanuzi wake kuhusu mwelekeo wakidiplomasia kati ya Kenya na Somalia.

Wakati huu akifunza kwenye Chuo Kikuu cha Riara, Idara ya Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa. Kabla ya hapo Februari 11, 2020 alinieleza jinsi alivyojaribu kunitumia fedha na badala yake zikamfikia kimakosa jamaa laghai, wakati akijaribu kumpigia simu hapokei.

Harakati za kujaribu kufikia Safaricom kumrejeshea fedha hizo hazikufua dafu, zilikuwa tayari zimetumika. Kumsisitizia kuwa tuandikishe taarifa kwa polisi, Prof. alinieleza “Wandera, uchumi wa Kenya umewabana wengi, watu wamekuwa wahuni, tusimlaumu.”

Wengi wakiendelea kumuomboleza mwandishi wa riwaya ya ‘Siku Njema’, ‘Mbaya Wetu’, ‘Kidagaa Kimemwozea’, ‘Pepela na Mto’ ‘Ndoto ya Almasi’ miongoni mwa vitabu vingine, mimi daima nitajivunia na kusherehekea muda niliotangamana naye.

Kennedy Wandera, ni Mwandishi wa Habari, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, VOA, jijini Nairobi, Kenya.