Safiri salama mwalimu na mlezi wangu wa lugha – Wangu Kanuri
Na WANGU KANURI
“Wema, utu, upole, ukarimu na utendakazi,” ndizo sifa zake marehemu Prof Ken Walibora. Waliotangamana naye kwa uhakika watakiri haya.
Profesa alikuwa mtetezi wa lugha ya Kiswahili, mwandishi shupavu aliyehakikisha kuwa Kiswahili kimepewa hadhi.Isitoshe, uandishi wake wenye mnato ulimfanya kuzamia katika utunzi wa riwaya, hadithi fupi, mashairi na hata tamthilia.
Mswada wake ambao kabla ya kifo chake alikuwa akihariri ulikuwa wenye kuangazia uhasama kati ya watu wa ukoo mmoja.
‘Jela ya Kitinda Mimba’ ni hadithi fupi teule ambayo nilipata kuisoma. Kauli yake kuu, ‘atingishe kibiriti aone kama ndani mna njiti,’ ilijitokeza katika hadithi fupi hiyo na katika kitabu chake kingine, ‘Kidagaa Kimemwozea’.
Profesa alikuwa na maono ya kuhakikisha kuwa uandishi bunifu umeng’aa haswa nchini Kenya huku akisisitiza kuwa sharti waandishi chipukizi wajiandae katika kuhakikisha uandishi wao una mnato.
Isitoshe katika nusura kila tanzu za fasihi simulizi alikuwa na haya ya kusema: Katika uandishi wa hadithi fupi zingatia tukio moja peke yake. Katika uandishi wa mashairi, lenga ubunifu wa hali ya juu wa kichwa cha shairi na mtiririko usio mgumu sana kueleweka.
Mwishowe, katika uandishi wa riwaya, hakikisha kuwa hadithi inaonyesha mtiririko wa mawazo ya mwandishi na hamna pahala ambapo panavuja.Marehemu Prof Walibora alikuwa na ari ya kuwasaidia waandishi chipukizi ambao waliipenda lugha ya Kiswahili.
Jambo hili lilimpa moyo kwani alijua baadaye Kiswahili hakitaangamia bali kitazidi kukua.Moyo wake pia uliwaendea wanawake ambao alisema kuwa wameadimika katika ukuzaji wa lugha ilhali nafasi ya wanawake katika Kiswahili ipo.
Marehemu Profesa alinieleza hivi: “Wangu ukitaka kuwa mwanasoka shupavu, umtazame yule aliyebobea kisha uende uwanjani ufanye mazoezi.”
Hii ikawa kauli mbiu kwangu kuwa nijapotaka kuwa mwandishi mkomavu, basi lazima nivisome vitabu vya walionitangulia kisha nijitose katika uwanja wa uandishi na niandike.
Kwa maneno hayo, mwendazake Prof Walibora akanipa changamoto la kuibuni hadithi fupi. Isitoshe, alinipa nakala ya ‘Kicheko cha Ushindi’ huku akisisitiza kuwa iwapo ningetaka kubobea katika uandishi wa hadithi fupi sharti nisome kitabu hicho.
Nikajitosa uwanjani, na kwa kufuata maagizo, nikaibuni ‘Risasi ya Kujua’ na kumtumia mwendazake lakini akaondoka duniani kabla hajaisoma hadithi hiyo.
Mengi tulijadili, ushauri mwingi ukanipa na hakika mshumaa wa kukuza Kiswahili kamwe hautazimika. Ulikuwa kwangu shujaa na kiongozi wa kupigiwa mfano. Mungu ailaze roho yako pahala pema peponi.”