Lamu yaanza kufufua visima vya kale
NA KALUME KAZUNGU
SERIKALI ya Kaunti ya Lamu imeanzisha mpango wa kufufua visima vya kale, ikiwemo vile vya miaka 100 na zaidi ili kuongeza kiwango cha usambazaji maji eneo hilo katika harakati za kukabiliana na janga la Covid-19.
Afisa Mkuu wa Idara ya Masuala ya Huduma za Jamii, ambaye pia anasimamia Idara ya Biashara, Utalii, Uwekezaji na Utamaduni eneo hilo, Atwa Salim, alisema kufikia sasa tayari wametambua visima vipatavyo 15 kwenye maeneo ya Kibaki Grounds, Jua Kali, Kinooni, Kanu, Manda-Okoe, Langoni, Gadeni, Kashmir na sehemu zingine ambapo tayari shughuli ya kuvifufua visima hivyo inaendelea.
Aliwataka wananchi kote Lamu kutoa ripoti kwa idara yake endapo wako na ufahamu wa visima zaidi vinavyohitaji kufufuliwa ili kuongeza usambazaji maji eneo hilo.
“Kutokana na kupanda kwa uhitaji wa maji ambayo msimu huu wa Corona yanatumika kwa wingi ili kudumisha usafi wa miili na mazingira yetu, serikali ya kaunti imeafikia kufufua visima vyote vya kale vilivyosahaulika.
“Tuko na visima vingi eneo hili ambavyo vimedumu kwa zaidi ya karne moja lakini bado viko na maji safi. Tumeamua kuvisafisha ili kutoa maji kwa mitaa inayokabiliwa na changamoto za rasilimali hiyo. Wakazi, ikiwemo maskini watakuwa wakipata maji ya bure kutoka kwa visima hivyo. Tayari tumeanza kushughulikia visima vipatavyo 15 eneo hili,” akasema Bw Salim.
Meneja wa Bodi ya Kusambaza Maji, Kaunti ya Lamu (LAWASCO), Bw Paul Wainaina, alisema ofisi yake inashirikiana kwa karibu na serikali ya kaunti katika mpango huo wa kufufua visima vya zamani.
Alisema juma hili ofisi yake itatoa dawa za kutibu visima vyote vitakavyofufuliwa ili kutoa maji ya kusaidia kukabiliana na Coronavirus.
“Tunashirikiana kufanikisha mpango huo wa kufufua visima vya kale kote Lamu. Juma hili LAWASCO itatoa dawa aina ya chlorine ili kunyunyiza visima vyote vitakavyofufuliwa ili maji yawe salama kwa matumizi ya binadamu,” akasema Bw Wainaina.
Kwa upande wake, Afisa msimamizi wa mradi huo wa ufufuzi wa visima vya kale, Abdulaziz Sadique, aliusifu mpoango huo wa kaunti, akisema utasaidia pakubwa watu wa tabaka la chini kupata maji kwa urahisi.
Miongoni mwa wanaolengwa kunufaika na mradi huo ni wahudumu zaidi ya 200 wa soko la manispaa ya Lamu ambao hivi majuzi walihamishwa kutoka eneo la Mkunguni hadi Kibaki Grounds katika harakati za kutafuta nafasi mwafaka ya wanabiashara kudhibiti umbali wa mita moja ili kuepuka maambukizi ya Covid-19.
“Mahali kama vile Kibaki Grounds kumekuwa na changamoto ya maji. Eneo lile hata hivyo limezingirwa na visima vingi vya kale. Ninaamini vikifufuliwa wahudumu 200 walioko sehemu ile watanufaika pakubwa,” akasema Bw Sadique.