• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Kwaheri Walibora, wengi tutakupeza

Kwaheri Walibora, wengi tutakupeza

Na OSBORNE MANYENGO

MWANDISHI mahiri na mwanahabari mbobevu, Prof Ken Walibora hatimaye alizikwa jana nyumbani kwao eneo la Bonde, Suwerwa, kilomita nne kutoka Makutano kwa Ngozi, Cherang’any, Kaunti ya Trans Nzoia.

Mwili wa Prof Walibora uliwasili nyumbani kwao saa nane na dakika 26 na kupokelewa kwa majonzi makuu na familia na marafiki, wote kwa jumla wakiwa watu 15.Ibada ya mazishi hayo ilichukua dakika 47.

Mwili wa mwendazake uliwasili ukisindikizwa na msafara wa magari manne pamoja na gari la walinda usalama.

Bango kubwa lenye picha yake lilikuwa limeandikwa, Always in Our Herats…. Even if ink has run dry love lives on…Kwaheri Yaya, yaani “Utasalia mioyoni mwetu daima… Hata kama wino umekauka, upendo wetu haunyauki… Kwaheri Ndugu”.

Baada ya mwili wa jagina huyo wa fasihi ya Kiswahili kuteremshwa kaburini, nduguze na mamaye wa kambo walipewa fursa ya kuweka maua yenye mchanganyiko wa rangi za manjano, nyeupe na kijani kibichi kaburini.

Ingawa hakukuwa na watu wengi, kutokana na kanuni za Wizara ya Afya kama njia ya kukabili maambukizi ya corona, hakukukosekana wasomi wenzake na wapenzi wa lugha ya Kiswahili.

Miongoni mwao walikuwa Afisa wa Mawasiliano wa Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH), Bw Hezekia Gikambi, Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kibabii, Prof Odeo Ipapa, Katibu wa chama cha Kiswahili Afrika Mashariki, Prof Inyani Simala, mwenyekiti wa chama cha Chakita, Dkt Mausal Kandagos, mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Laikipia, Dkt Sheila Wandera, aliyekuwa mwenyekiti wa UASU, Prof Sammy Kubasu na Mwalimu Kennedy Anduvate aliyewakilisha chama cha walimu wa Kiswahili wa shule za msingi.

Bw Gikambi ambaye pia alikuwa rafiki wa dhati wa Prof Walibora, alisema rafikize na wataalamu wa Kiswahili waterejea hapo baada ya janga la corona kuisha kumwaga rasmi.

“Wataalamu wa Kiswahili, waandishi wa vitabu na rafikize wengi walitaka sana kuhudhuria mazishi haya lakini kutokana na kanuni za wakati huu, tumepanga kwamba punde janga la corona likiisha, tutakusanyika tuje tulizuru kaburi lake,” akasema.

Mbali na hayo, alisema wenzake watapanga kongamano la kuzindua kitabu cha kumkumbuka marehemu Walibora.

Inadaiwa kwamba Prof Walibora aliaga dunia mnamo Aprili 10, 2020 katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) alikokimbizwa baada ya kugongwa na basi la ‘Double M’ katika barabara ya Landhies, Nairobi karibu na kituo cha mabasi cha Machakos Country Bus.

Utata kuhusu kifo chake ulizuliwa na ripoti ya upasuaji wa maiti iliyotolewa na mwanapatholojia mkuu wa serikali, Johansen Oduor, aliyethibitisha kwamba kulikuwa na majeraha kwenye upande wa kulia wa kichwa, huku mkono wa kulia ukiwa umevunjika na damu kuvuja ubongoni.

Kulikuwa na jeraha la mkono wa kulia ambao ulionyesha kwamba alikuwa amedungwa kwa kisu.Ni madai haya yaliyomfanya kaka yake marehemu, Mwalimu Patrick Lumumba atoe wito kwa serikali ichunguze kwa kina na kujua kilichosababisha mauti ya nduguye.

Jana kitengo cha upelelezi wa jinai (DCI) kiliashiria kuwa kuna uwezekano mkubwa Prof Walibora aliuawa katika mzozo na mchapishaji wa vitabu.

“Tunaamini serikali ina uwezo wa kuchunguza na kutatua fumbo kuhusu mauaji na ndugu yangu. Tunaomba uchunguzi huo ufanywe kwa makini ili umma upewe majibu,” akasema.

You can share this post!

Polo aona moto kuchezea maski

Wawili waangamia kwa mafuriko Samburu

adminleo