• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:15 PM
Rais ahakikishia taifa mitihani ya kitaifa itafanywa mwaka huu

Rais ahakikishia taifa mitihani ya kitaifa itafanywa mwaka huu

Na SAMMY WAWERU

Rais Uhuru Kenyatta amehakikishia taifa kuwa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane, KCPE na kidato cha nne, KCSE, 2020 sharti ifanywe mwishoni mwa mwaka.

Aidha, Rais Kenyatta ameondoa shauku kuwa huenda ikaahirishwa hadi mwaka ujao, 2021 kufuatia athari za janga la Covid – 19 ambalo halijulikani litadumu kwa muda gani.

Amesema wakati unaoratibiwa mitihani kufanywa ukifika, mikakati itatolewa. “Wakati huo ukifika tutatoa mipangilio ya mambo na ratiba,” Rais akasema mapema Jumatano kwenye mahojiano ya pamoja na vituo vya redio vinavyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiswahili.

Kiongozi wa nchi pia amewataka watahiniwa wa mwaka huu, 2020 kuendelea kujiandaa kwa zoezi hilo. “Wadau husika katika sekta ya elimu waendelee kutayarisha watoto wetu, lazima wafanye mitihani ya kitaifa,” akahimiza.

Mwezi uliopita, Machi, taasisi zote za elimu nchini zilifungwa kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona nchini. Rais Kenyatta alichukua hatua hiyo ili kuzuia maambukizi zaidi.

Mikusanyiko ya umma, ikiwamo ibada za kidini, mabaa na burudani, pia ilipigwa marufuku kwa muda. Hafla za mazishi na harusi zinahudhuriwa na idadi ndogo ya watu na kutakiwa kufanywa kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Wanafunzi sasa wananolewa bongo kupitia mitandao na vipindi vinavyopeperushwa kupitia runinga na mitihani kuchapishwa kwenye magazeti. Ni hali inayozua wasiwasi kuhusu maandalizi ya kutosha kwa watahiniwa wa mitihani ya kitaifa 2020.

Kwenye mahojiano hayo yaliyopeperushwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya Nairobi, Rais Kenyatta amewataka wanafunzi kujua Covid – 19 haijaathiri sekta ya elimu pekee, ila sekta zote na ulimwengu kwa jumla.

You can share this post!

Uhuru awaomba malandilodi kuwa na utu

Jiji la Nairobi lingali chafu chini ya usimamizi mpya

adminleo