• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Tutawanyaka wote waliotoroka karantini – Uhuru

Tutawanyaka wote waliotoroka karantini – Uhuru

Na WANDERI KAMAU

WATU 50 ambao walitoroka kutoka Chuo cha Mafunzo ya Matibabu (KMTC) jijini Nairobi, watasakwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ameonya Rais Uhuru Kenyatta.

Watu hao walitoroka kutoka chuo hicho mnamo Jumatatu usiku kwa kuruka ua wake, baada ya kula chakula cha jioni.

Taasisi hiyo inatumika kama mojawapo ya vituo vya kuwahifadhi watu wanaohofiwa kuambukizwa virusi hivyo katika Kaunti ya Nairobi.

Kauli hiyo inajiri huku watu kadhaa waliotoroka wakikamatwa katika kaunti za Nairobi na Kericho.

Kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio Jumatano, Rais Kenyatta alisema kuwa msako mkali dhidi yao tayari umeanza, ambapo watasakwa na kuadhibiwa vikali.

“Hatuwezi kuruhusu watu wachache wasiojali kuhatarisha maisha ya mamilioni ya Wakenya. Maafisa wa usalama tayari wameanza kuwasaka, ambapo tunaamini kwamba watakamatwa na kuadhibiwa,” akasema Rais.

Baadhi ya watukatika vituo hivyo wamekuwa wakilalamikia gharama ya kuhusu masuala kama chakula na malazi.

Wiki iliyopita, baadhi ya watu walio kwenye karantini katika Chuo Kikuu cha Kenyatta walitishia kugoma lakini juhudi zao zikazimwa na polisi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Matibabu nchini, Dkt Patrick Amoth, alikuwa amesema kuwa serikali itashughulikia malalamishi hayo. Wengi wanalalamika kuwa ahadi hiyo bado haijatekelezwa.

Wakati huo huo, Rais aliondoa uwezekano wowote wa serikali kulegeza masharti ya kafyu na marufuku ya kutotoka nje katika baadhi ya maeneo nchini, akisema kuwa hilo litalingana na matokeo ya muda uliowekwa.

Hili linafuatia ombi la baadhi ya viongozi wa Kiislamu kwa Rais Kenyatta kuwaruhusu kuendesha sherehe za Sikukuu ya Idd Ul-Fitr kama kawaida, ambapo huwa wanajumuika pamoja.

Hata hivyo, Rais alikataa mwito huo, akiwaeleza kuwa hata Wakristo walibaki majumbani mwao wakati wa sherehe za Sikukuu ya Pasaka, ambayo ni mojawapo ya sikukuu kubwa zaidi kwenye kalenda yao.

“Ikiwa tutamruhusu kila mtu kuendesha shughuli zake atakavyo, basi imanaanisha kuondoa kanuni ambazo tayari tumeweka kuhusu virusi hivi. Tutafanya hivyo tu kulingana na mashauri tutakayopata kutoka kwa wataalamu,” akasema.

Kufikia sasa, kuna zaidi ya Wakenya 2,000 ambao wamo katika vituo hivyo, ambapo wengi wao ni wale waliowasili kutoka ughaibuni.

You can share this post!

Duma na simba waambukizwa virusi vya corona na binadamu

Wizara ya Afya yafundisha Wakenya jinsi ya kuvalia barakoa

adminleo