Bei ya unga yapanda uhaba wa mahindi ukizidi
BARNABAS BII Na ONYANGO K’ONYANGO
WAMILIKI viwanda vya unga wa mahindi katika eneo la Magharibi, wamesitisha shughuli na kuwafuta kazi wafanyakazi kutokana na uhaba wa mahindi.
Hatua hiyo imesababisha kuongezeka kwa bei ya unga.
Wenye viwanda hao chini ya Muungano wa Wasagaji Mahindi (GBMA), jana walisema wanakabiliwa na changamoto za kupata mahindi sokoni baada ya wakulima wengi kumaliza hifadhi yao, huku serikali ikipanga kuagiza magunia milioni nne kufidia upungufu huo.
Bei ya mahindi imeongezeka kutoka Sh3,200 hadi Sh3,700 kwa kila gunia la kilo 90 katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Hii imewalazimu wamiliki viwanda vya kusaga mahindi kupunguza oparesheni zao kwa sababu ya gharama.
“Wafanyikazi zaidi wanatazamiwa kufutwa kazi kwa kuwa viwanda vingi havina mahindi,” alisema Bw Kipngetich Mutai, Mwenyekiti wa GBMA.
Bei ya unga wa mahindi imeongezeka kutoka Sh110 hadi Sh130 kwa kila pakiti ya kilo mbili katika maduka mengi.
Wamiliki viwanda hao wamesema kuna uhaba mkubwa wa mahindi katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hali hiyo inatokana na kudidimia kwa uzalishaji wa zao hilo msimu uliopita kutokana na mabadiliko ya hali ya anga.
Mazao ya mahindi nchini yalipungua kutoka magunia 44 milioni hadi 33 milioni huku kiwango kinachovunwa kikitazamiwa kupungua hata zaidi msimu huu.
Wakulima wanasema uvamizi wa nzige umetatiza shughuli ya upanzi katika maeneo makuu ya ukuzaji mahindi.
Wasagaji wameihimiza serikali kuharakisha uagiziaji wa mahindi ili kuzuia uhaba zaidi.
wa zao hilo ammbao umesababisha bei kupanda pakubwa, hali inayoashiria kuongezeka kwa bei ya unga.
Wanaitaka serikali kuondoa vikwazo vya biashara baina ya mipaka ili kuwezesha kuingia bila kutatizwa kwa mahindi nchini kutoka mataifa jirani huku bei ikifikia Sh3,200 kwa kila gunia la kilo 90 kutokana na kudidimia kwa zao hilo.