• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Gavana aweka mikakati kukabili Covid-19 Kiambu

Gavana aweka mikakati kukabili Covid-19 Kiambu

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kaunti ya Kiambu wameshauriwa kufuata ushauri wa serikali kuepuka athari hasi za homa hatari ya corona.

Gavana wa eneo hilo Dkt James Nyoro, alisema Alhamisi kaunti yake imeweka mikakati inavyostahili ili kupambana na janga hilo.

Wakati wa hafla hiyo alizindua gari jipya la zimamoto, lenye thamani ya Sh60 milioni.

Alisema gari hilo kutoka nchini Austria lina uwezo wa kutekeleza majukumu mengi wakati mmoja.

Alizindua mradi huo mnamo Alhamisi katika afisi kuu ya kaunti mjini Thika alipotoa mwelekeo na mpangilio wa serikali yake katika siku zijazo.

Gavana huyo alisema wanalenga kuwalisha familia 10,000 katika kaunti mzima ya Kiambu.

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba familia hizo zinapata chakula cha mwezi moja mfululizo. Tunawapongeza wahisani wote ambao wamejitolea kusaidia familia zilizoathirika,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba soko za Gacharage, Ndenderu,na Ruaka zinapulizwa dawa ili kuzuia viini vya Corona.

Alisema tayari hospitali ya Tigoni itakuwa na vitanda 102 vya wagonjwa watakaotengwa huko kwa homa ya Corona.

Alitaja kiwanda kimoja mjini Kikuyu ambacho kinaendelea kushona barakoa 20,000 kwa siku chache zijazo ili kuwapa wakazi wa Kiambu.

Alisema hospitali ya Kijabe itapata vifaa 16 vya kusambaza hewa – ventilators – na kuhimiza hospitali za wamiliki binafsi kujitokeza ili kusaidia zinakoweza.

Alisema Chuo cha Kiambu Institute of Technology, na Kikuyu University Campus, watapata vitanda 50 kwa kila moja ili kugeuzwa vituo vya karantini.

Nazo hospitali za Karuri na Thika Medical College zitapata vitanda 100 kwa wagonjwa wa Covid-19.

Alitoa mwito kwa wananchi wazingatie mambo matatu muhimu ili kukabiliana na janga hilo la Covid- 19.

Mambo hayo ni kunawa mikono kuvalia barakoa, na kuketi mbali na mwingine kwa mita moja au zaidi.

Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro akizindua gari jipya la zimamoto mjini Thika Aprili 23, 2020. Picha/ Lawrence Ongaro

Naibu kamishna wa Thika Magharibi, Bw Douglas Mutai, alisema kamati ya watu 12 itaendelea kufuatilia usambazaji wa chakula katika kaunti nzima ya Kiambu.

“Tutahakikisha kila mkazi wa Kiambu aliyeathirika na makali ya njaa anapata msaada wa chakula. Tutakuwa na uwajibikaji tukiendesha shughuli hiyo,” alisema Bw Mutai.

Alitoa mwito kwa watakaopokea msaada huo wa chakula kuutumia kwa makini.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na spika wa bunge la kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu, naibu gavana Bi Joyce Ngugi, mwenyekiti wa wafanyabiashara Bw Alfred Wanyoike na washikadau wa kaunti ya Kiambu.

You can share this post!

Ramadhani yaanza bila sherehe za kawaida

Msimu wa ligi kuu ya Uholanzi wafutiliwa mbali

adminleo