TAHARIRI: Tuunge yeyote yule anayekabili corona
Na MHARIRI
KUFIKIA Jumanne maambukizi ya virusi vya corona yaliongezeka na kufika jumla ya watu 374.
Hii ilikuwa ni baada ya watu 11 zaidi kuripotiwa kuambukizwa. Kati ya kumi na mmoja hao, saba walitoka Nairobi kisha wanne ni kutoka Mombasa.
Hata hivyo, katika habari za kutia moyo ni kwamba, juma hili idadi ya watu wanaopona kutokana na maradhi ya Covid-19 imeanza kuongezeka.
Hii ni ishara nzuri ingawa haifai kutufanya tuanze kuendekeza uzembe katika utekelezaji wa kanuni zilizopendekezwa na Wizara ya Afya.
Siku ya Jumatatu Wakenya wanane walipona kisha hapo jana watu wengine 10 walipona.
Cha kupendeza zaidi kwa mujibu wa takwimu zinazoendelea kutolewa kila siku ni kwamba, sasa idadi ya wanaopona ni sawa na wanaoambukizwa. Awali idadi ya maambukizi ilikuwa juu sana na hakukuwa na waliokuwa wanapona.
Ubashiri uliokuwa umetolewa awali kwamba kufikia mwisho wa mwezi wa Aprili Wakenya takriban 10,000 wangalikuwa wameambukizwa Covid-19 pia umeambulia pakavu.
Ubashiri huo pamoja na hali ya kutisha ya maafa katika mengi ya mataifa ya uzunguni ni hali iliyotuchorea taswira ya kutisha.
Licha ya mataifa mengi ya Afrika kuwa na miundomsingi dhaifu katika sekta ya matibabu, tunashukuru Mungu kwamba nakama hii ya corona haijatubwaga.
Tunapofurahia ufanisi huu mdogo tulioupata hadi kufikia sasa, hatufai kulegeza kamba katika juhudi zetu kukabili janga hili la corona.
Huu ni wakati ambapo tunafaa kukuza mshikamano wa hali ya juu na kufaana kwa hali na mali. Inapendeza kwamba hadi kufikia sasa tumewaona watu binafsi na pia mashirika yakijitokeza kuwafaa waathiriwa wa corona mbali na kupiga jeki juhudi za serikali katika vita hivi dhidi ya adui huyu asiye na tiba.
Ni kwa mintarafu hii ambapo inasikitisha kwamba licha ya gavana Mike Sonko wa Nairobi kujitolea kusaidia wakazi kwa namna ya kuwa na vituo maalum vya kueua watu wanaoingia jijini pamoja na vitongoji vyake, wapo watu waliovibomoa.
Hata hivyo, tunashukuru mahakama kwa kutoa agizo Jumanne la kusitisha ubomoaji wa vituo hivyo hadi kesi iliyowasilishwa na gavana Sonko itakaposikilizwa.
Huu si wakati kutumia nguvu zetu katika mambo ambayo yatahatarisha maisha ya Wakenya. Hisani inapotolewa tuipokee kwa nia safi.
Tofauti za kisiasa, kimrengo na kiimani hazimsaidii Mkenya wa kawaida kwa sasa. Jameni Wakenya tuvute kuelekea kumoja ndipo tufaulu katika kukabili maradhi ya Covid-19.