• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wito klabu zitengewe asilimia kubwa mgao wa fedha za Fifa

Wito klabu zitengewe asilimia kubwa mgao wa fedha za Fifa

Na CHRIS ADUNGO

HUKU kila mojawapo ya mashirikisho ya soka duniani yakitarajiwa kupokea kima cha Sh50 milioni kutokana na mgao wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) limeombwa kutengea vikosi vya soka vinavyopitia hali ngumu asilimia kubwa ya fedha hizo.

Kwa mujibu wa washikdau mbalimbali, hatua hiyo itasaidia kuinua kiwango cha mapato ya klabu kadri zinazovyojitahidi kujikimu wakati huu wa janga la corona.

Mwenyekiti wa zamani wa Nzoia United, Yappets Mokua amesema kwamba vikosi vingi vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) vinahitaji zaidi fedha hizo wakati huu kuliko kipindi chochote kingine.

“Pendekezo langu ni kwa fedha hizo zigawiwe klabu kwa kiwango cha 80:20. Asilimia 80 ya fedha itolewe kwa vikosi na asilimia 20 nyingine isalie katika hazina ya FKF kwa minajili ya kuendesha masuala muhimu ya usimamizi,” akatanguliza Mokua.

“Fedha za klabu pia zitolewe kwa mgao wa 80:20 ambapo asilimia 80 zinafaa zitumike kuwadumisha maafisa na wachezaji kimshahara na asilimia 20 nyingine itengewe masuala ya usimamizi kwa kuwa vikosi vitahitaji mipira, neti na vifaa vingine soka ya humu itakaporejelewa,” akaongeza kinara huyo.

Huku kukukosekana mwafaka kuhusu namna ambavyo msimu huu wa 2019-20 unavyofaa kukamilishwa hasa katika KPL, mapendekezo mbalimbali yanazidi kutolewa na washikadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Mokua amesisitiza haja ya kukumbatiwa kwa kanuni zilizopo ili kutoa mwongozo kuhusu namna ambavyo mshindi wa KPL atatawazwa, vikosi vitakavyoshushwa ngazi na vingine kukwezwa ngazi iwapo janga la corona litavuruga kabisa juhudi za kurejelewa kwa kampeni za muhula huu.

“Sheria ni bayana kuhusu namna jamvi la msimu huu katika soka ya Kenya linavyostahili kukunjwa rasmi. Kwa mujibu wa sheria, iwapo chini ya asilimia 50 ya mechi hazijachezwa, basi msimu mzima unafaa kufutiliwa mbali,” akatanguliza.

“Iwapo kati ya asilimia 50 na zaidi ya mechi zimesakatwa, basi mshindi aamuliwe kutokana na jinsi msimamo wa jedwali ulivyo,” akasema.

Hadi kivumbi cha KPL kilipoashirishwa mwanzoni mwa Machi 2020, Gor Mahia walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 54, mbele ya Kakamega Homeboyz na Tusker FC wanaofunga mduara wa tatu-bora.

Huku baadhi ya ligi kuu za bara Ulaya zikishirikiana na serikali za mataifa yao kufanikisha marejeo ya michuano ya soka licha ya mlipuko wa corona, vinara wa KPL bado hawajatoa mwongozo kuhusu namna msimu huu utakavyotamatishwa.

You can share this post!

Bingwa wa ujasiri wa kuzungumza na kujieleza mbele ya umma

Wabunge wataka amri ya kafyu isiwaguse

adminleo