• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
PSG watawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa

PSG watawazwa mabingwa wa ligi kuu ya Ufaransa

Na CHRIS ADUNGO

PARIS Saint-Germain (PSG) wametawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) siku chache baada ya serikali ya taifa hilo kutangaza kwamba isingewezekana kwa kampeni za soka msimu huu kurejelewa kutokana na janga la virusi vya corona.

Hadi kufutiliwa mbali kwa kipute cha Ligue 1, PSG walikuwa wakiselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 12 zaidi kuliko Olympique Marseille ambao wanakamata nafasi ya pili kwa pointi 56.

Shughuli zote za soka nchini Ufaransa ziliahirishwa kwa muda usiojulikana mnamo Machi 13, 2020.

Mapema wiki hii, Serikali ya Ufaransa ilifutiliwa mbali msimu huu mzima wa 2019-20.

Pindi baada ya kutangazwa wafalme wa soka ya Ligue 1 kwa mara nyingine msimu huu, PSG walisema kwamba ushindi huo ni zawadi muhimu kwa maafisa wote wa afya ambao wamekuwa wakijishughulisha vilivyo katika vita vya kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Mwenyekiti wa PSG, Nasser Al-Khelaifi alitambua pia ukubwa wa mchango na kujitolea kwa maafisa wa afya ambao wamejinyima mengi katika kipindi cha wiki nyingi zilizopita za kukabiliana na corona.

“Tunaelewa, kuheshimu na kuunga mkono maamuzi ya Serikali ya Ufaransa ya kutamatisha msimu huu wa soka. Sawa na inavyosisitizwa na serikali, tunaamini kwamba afya ni jambo muhimu zaidi linalostahili kupewa kipaumbele na kila mmoja,” akatanguliza kinara huyo.

“Katika kipindi hiki kigumu, naamini kwamba ubingwa huu wa Ligue 1 utaleta chembechembe za furaha na matumaini kwa mashabiki wetu ambao ningependa kuwashukuru wote kwa upekee wa mchango wao katika mafanikio ya kila msimu ya PSG,” akaongeza.

Kabla ya Serikali ya Ufaransa kufikia maamuzi ya kufutilia mbali msimu huu mzima, vinara wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo walikuwa wakitarajia kurejelea kampeni za muhula huu mnamo Juni 17.

Huku PSG wakitawazwa mabingwa kutokana na wingi wa alama zao hadi kufikia sasa, Lorient nao wamepokezwa ubingwa wa Ligi ya Daraja ya Kwanza (Ligue 2) nchini Ufaransa.

Lorient walikuwa wakijivunia alama 54, moja pekee kuliko Lens ambao ni wa pili wakati kivumbi cha Ligue 2 kilipofutiliwa mbali vilevile. Vikosi hivyo viwili vimepandishwa daraja kujaza nafasi za Amiens na Toulouse ambao wameshushwa ngazi kwenye kipute cha Ligue 1.

Olympique Lyon ambao walikuwa katika nafasi ya tano wiki moja kabla ya mchuano wa mwisho wa msimu huu, walirushwa hadi nafasi ya saba. Kikosi hicho kwa sasa kimesema kwamba kitakata rufaa dhidi ya maamuzi ambayo yameafikiwa na serikali kwa ushirikiana na vinara wa soka ya Ufaransa.

Hatua yao inachochewa na pigo la kukosa kuwa sehemu ya vikosi vitakavyowania ubingwa wa Europa League msimu ujao.

Kwa mujibu wa Lyon, wao wana haki ya kufidiwa mabilioni ya fedha ambazo vingenevyo wangezitia mfukoni kwa kufuzu kwa kipute cha Europa League iwapo msimu ungekamilishwa jinsi ilivyotarajiwa.

“Ingawa tunatarajia rufaa nyingi, maamuzi yetu yanasalia hivyo yalivyo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa ligi za soka nchini Ufaransa (LFP), Didier Quillot.

Awali, LFP ilikuwa na hadi tarehe 25, Mei 2020 kuwasilisha kwa vinara wa soka ya bara Ulaya (Uefa) majina ya vikosi ambavyo vinatarajiwa kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Europa League muhula ujao.

Hiyo ndiyo siku ambapo pia vinara wa Ligi Kuu zote za bara Ulaya walitarajiwa kuelezea Uefa iwapo watakamilisha kampeni za msimu huu au kuzifutilia mbali.

You can share this post!

Kampuni ya Capwell Thika yaweka mikakati ya kukabiliana na...

AGUERO: Wachezaji wanaogopa kurejelea EPL

adminleo