Michezo

Polisi wataka mamlaka ya kusitisha EPL iwapo watashindwa kudhibiti mashabiki

May 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

POLISI wa Uingereza wanataka wapewe ruhusa ya kufutilia mbali soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu iwapo mashabiki hawatazingatia kanuni mpya za afya pindi michuano hiyo itakaporejelewa baada ya janga la corona kudhibitiwa.

Haya ni kwa mujibu wa afisa mkuu wa polisi nchini Uingereza, Mark Roberts aliyehojiwa na gazeti la ‘The Daily Telegraph’.

Roberts ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha polisi wanaosimamia usalama wa washidakau wa soka nchini Uingereza, amesema hakuna mashabiki watakaoruhusiwa kukongama nje ya viwanja kabla, baada na wakati ambapo mechi zitakuwa zikiendelea katika kipindi hiki ambapo virusi vya corona bado ni tishio kubwa.

“Ambacho tusingependa kushuhudia ni hali ambapo mashabiki wanavunja kanuni zilizowekwa katika juhudi za kukabilia na maambukizi zaidi ya virusi hivi,” akatanguliza Roberts.

“Itakuwa heshima kubwa kwa maafisa wetu wa afya iwapo mashabiki watatii sheria na maagizo kutoka kwa wadau mbalimbali hadi msimu huu wa EPL ukamilike kwa mujibu wa taratibu zitakazowekwa.”

“Kadri sheria zinavyoheshimiwa ndivyo inavyokuwa rahisi kwa maazimio ya msimu huu katika ulingo wa soka kutimia. Vinginevyo, tungependa kupewa mamlaka ya kusitisha kabisa kivumbi hicho iwapo tutashindwa kuwadhibiti mashabiki” akaongeza.

Ligi Kuu ya EPL ilisitishwa mnamo Machi 13, 2020, kutokana na janga la corona ambalo limetikisa pakubwa ulingo wa michezo duniani kote.