Kimataifa

COVID-19: Magufuli avitilia shaka vipimio vinavyotumika nchini Tanzania

May 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

RAIS wa Tanzania John Magufuli amedai vipimio (test kits) vinavyotumika kupima homa ya corona nchini humo vina kasoro.

Akiongea Jumapili alisema vifaa hivyo vimetoa matokeo ya uwepo kwa virusi vya corona hata katika sampuli zilizokusanywa kutoka kwa kondoo na papai.

Magufuli ambaye serikali yake imekosolewa kwa kutoweka masharti makali ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, amewahi kuwahimiza Watanzania kutegemea maombi kama kinga dhidi ya ugonjwa huo.

Lakini Jumapili alidai vipimio vinavyotumika kupima watu kubaini ikiwa wana virusi hivyo vina “hitilafu za kiufundi”.

Akihutubu katika shughuli fulani mjini Chato, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, Rais Magufuli alidai kuwa mitambo hiyo iliagizwa kutoka nje.

“Nimeagiza maafisa wa usalama kukagua mitambo hiyo ili kuibaini viwango vyayo vya ubora,” akaeleza.

Akaongeza: “Kwa sababu mitambo hii imegundua kwamba sampuli kutoka kwa papaya na kondoo zina virusi vya corona, huenda baadhi ya watu wanadaiwa kuwa virusi hivyo kwa hakika hawana.”

Alisema kuwa kuanzia sasa Tanzania itakuwa makini inapopokea misaada ya vifaa na mitambo mbalimbali kutoka ng’ambo.

“Kuna ukora unaoendelea hapa. Nilisema hapo awali kwamba hatupaswi kukubali misaada yote na kuamini kuwa ni salama kwa taifa letu,” Magufuli akasema akiongeza kuwa mitambo hiyo sharti ichunguzwe kwa kina.

Mnamo Jumapili, Tanzania iliandikisha visa 480 vya maambukizi ya Covid-19 na vifo 16.