Habari Mseto

Serikali kuwaondoa kwa lazima walioko katika 'ngome' za mafuriko

May 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imesema haitaki kubembeleza watu wanaokatalia maeneo hatari na yanayoshuhudia mafuriko, kutokana na athari za mvua kubwa inayonyesha. 

Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i alisema Jumatano serikali itatumia nguvu kuwaondoa na kuwapeleka maeneo salama.

“Ni heri tutumie nguvu kuokoa maisha ya watu. Kama serikali, tuna wajibu wa kulinda maisha ya kila Mkenya. Tusipofanya hivyo, tutakuwa tunahatarisha maisha ya wanaoishi maeneo yaliyoathirika na mafuriko,” Dkt Matiang’i akaweka wazi akiwa jijini Nairobi.

Watu wapatao 194 wamekufa maji kutokana na mafuriko na athari nyinginezo zinazohusiana na mvua kubwa inayoshuhudia maeneo tofauti nchini.

Baadhi ya mito imefurika na kuvunja kingo zake.

Mto Tana, Nyando na Nzoia, imevunja kingo zake na wanaoishi kandokando wametakiwa wahame mara moja.

Garissa, Tana River, Nyando, ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika pakubwa na mafuriko.

Akihakikishia taifa serikali inafanya kila iwezalo kuokoa maisha, waziri Matiang’i alisema shughuli za kuhamisha watu itaendelea kwa muda wa wiki mbili zijazo, kupitia ushirikiano wa maafisa wa usalama, shirika la msalaba mwekundu, serikali za kaunti zilizoathirika na wadau husika kuangazia majanga nchini.

“Shughuli za kuondoa watu kutoka maeneo hatari Garissa na Tana River zinaendelea. Tunaondolea kutoa tahadhari maeneo hatari,” waziri akasema.

Waathiriwa wanapelekwa katika shule mbalimbali katika kaunti zao, waziri akisema wataendelea kupokea misaada ya mahitaji ya kimsingi.

Serikali inapambana kudhibiti janga la Covid-19, na Dkt Matiang’i alikiri inapitia wakati mgumu kwa kile alitaja kama “raslimali kupungua” ikizingatiwa kuwa mafuriko pia yanahitaji fedha kushughulikia athari zenyewe.