Gavana Mutua apondwa kufungua ofisi ya kifahari wakati wa corona
Na BENSON MATHEKA
GAVANA wa Machakos Alfred Mutua amekashifiwa na Wakenya kwa kuanika ofisi yake mpya ya kifahari iliyogharimu Sh350 milioni wakati magavana wengine wanashughulika kukabiliana na janga la corona.
Wakenya kwenye mtandao walisema ingawa sio makosa kujenga ofisi, kinachohitajika wakati huu ni mikakati ya kupigana na corona na sio ofisi ya kifahari.
“Kujenga ofisi katikati ya janga kuwaonyesha kuwa haelewi kabisa mahitaji ya wakazi wa Machakos,” Alex Njuguna alisema kwenye Twitter.
Alisema jengo hilo lingekuwa hospitali ya kisasa kama iliyojengwa kaunti ya Kilifi kukabiliana na corona badala ya kutumia mahema katika uwanja wa michezo wa Kenyatta mjini Machakos kama hospitali ya muda.
“Mwambieni Gavana Mutua kwamba jengo hilo linafaa kuwa hospitali ya kutibu saratani, eneo la viwanda au chochote ambacho kinaweza kuletea watu wa Machakos mabadiliko katika maisha yao,” alisema Mkenya mwingine kwenye Twitter.
“ Wakati wa janga sio wakati wa maonyesho na sarakasi za uhusiano mwema anavyopenda Dkt Mutua,” alisema Hilda Kamene, mkazi wa Machakos.
Aibu
Alisema ni aibu kwa Gavana Mutua kuzindua ofisi ya kifahari huku wakazi wa kaunti yake wakikosa huduma bora za afya, maji safi na barabara nzuri.
“Kaunti ya Murang’a ilifungua hospitali mpya ya wagonjwa mahtuti. Kwetu Machakos tumekamilisha ujenzi wa ikulu yetu. Hamuwezi kuturingia,” mkazi mmoja alitania kwenye Twitter.
Ofisi hiyo ilianza kujengwa kabla ya janga la virusi vya corona kuripotiwa ulimwenguni.
Baadhi ya wakazi walimtetea Dkt Mutua wakisema amefanya mengi na ofisi hiyo sio mali yake binafsi.