Rai kocha mpya wa timu ya taifa ya hoki awadumishe nyota wa zamani
Na CHRIS ADUNGO
MVAMIZI wa Sikh Union, Davis Wanangwe amewataka makocha wapya wa timu ya hoki kudumisha idadi kubwa ya wachezaji walioshiriki mechi za mwaka jana za kufuzu kwa Olimpiki katika vibarua vijavyo.
Kwa mujibu wa Wanangwe, kikosi cha sasa cha magongo kinajivunia wanamagongo mahiri zaidi walio na uwezo na kiu ya kuvunia Kenya idadi kubwa ya mataji ya haiba.
Fidelis Kimanzi alipokezwa mikoba ya timu ya taifa mnamo Februari 2020 na Michael Malungu akateuliwa kuwa msaidizi wake. Ingawa hivyo, Kimanzi bado hajarasmisha kuteuliwa kwake.
Wanangwe ni mshindi mara tatu wa taji la Ligi Kuu ya Hoki ya Kenya. Alinyanyua ufalme huo mara mbili akivalia jezi za Strathmore na moja akiwa mchezaji wa Sikh.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 alistaafu rasmi katika ulingo wa hoki ya kimataifa mnamo 2014 baada ya kupata jeraha baya la goti lililomweka nje kwa msimu mzima.
Davis ambaye ni kakaye mshambuliaji Frank Wanangwe wa Butali Warriors, ametawazwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya Hoki kwa misimu mitatu tofauti.
“Ikilinganishwa na siku zangu za awali katika kikosi cha taifa, nahisi kwamba timu ya sasa ya Kenya inajivunia wachezaji wenye utajiri mkubwa wa vipaji na kiu ya kutwaa mataji,” akatanguliza Wanangwe.
“Kikosi kina idadi kubwa ya chipukizi na tuna kila sababu ya kutarajia makubwa kutoka kwao. Kinachohitajika tu kwa sasa ni kuwahimiza makinda hao washirikiana vilivyo na wachezaji wazoefu zaidi ambao wana tajriba pevu ili kikosi kisalie thabiti zaidi katika kila idara,” akaongeza.
Wanangwe alifunga mabao sita na kuibuka Mfungaji Bora wa kipute cha Kombe la Afrika mnamo 2011 chini ya kocha Meshack Senge.
Ingawa alijeruhiwa kwa mara ya kwanza mnamo 2011, alifanyiwa upasuaji mnamo 2014 baada ya jeraha hilo kuanza upya. Ilikuwa hadi 2018 alipojipa likizo ya miezi sita kabla ya kusalia tena nje ya ulingo wa hoki kuanzia Oktoba 2019.
“Kwa namna ambavyo hoki huchezwa, kupata majeraha ya magoti ni suala la kawaida mno. Kuna kuinama kwingi, jambo ambalo naamini huchangia majeraha mbalimbali ya misuli,” akasema Wanangwe kwa kusisitiza kwamba anapania kurejelea kampeni za msimu huu kwa matao ya juu zaidi kabla ya kuliangika rasmi gongo lake chini ya kipindi cha miaka mitatu ijayo.