Kimataifa

Obama akosoa hatua za serikali ya Trump kukabili Covid-19

May 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

WASHINGTON D.C., AMERIKA

RAIS wa zamani wa Amerika Barack Obama ameikosoa serikali ya Rais Donald Trump kuhusiana na hatua inazochukua kudhibiti maradhi ya Covid-19 akiitaja kama “isiyo na mpangilio wowote.”

Alisema hayo Jumamosi kwenye mawasiliano ya simu na watu ambao walihudumu katika utawala wake katika Ikulu ya White House.

Kauli ya Obama ndiyo yake ya kwanza kutoa dhidi ya utawala wa Trump na maafisa wake katika serikali ya sasa kuhusu jinsi wanavyokabiliana na janga la Covid-19.

Na huenda hii ndiyo maana anaamini kuwa wafuasi wa chama cha Democrat wanastahili kuunga mkono mgombeaji Joe Biden ili ashinde Trump katika uchaguzi wa urais wa Novemba 16, 2020.

Biden alihudumu kama Makamu wa Rais chini ya utawala wa Obama wa miaka minane kuanzia 2008 hadi 2016.

Katika mazungumzo hayo yaliyodumu kipindi cha nusu saa baina yake na Muungano wa Wahudumu wa Zamani wa Utawala wa Obama, Rais huyo wa zamani alisema kuwa hatua ambayo utawala wa Trump umechukua dhidi ya janga la corona ni kumbukumbu kuhusu haja ya uwepo wa serikali thabiti wakati kama huu mgumu.

Mazungumzo hayo yalilenga kuwahimiza wahudumu hao wa zamani chini ya utawala wa Obama kupiga jeki kampeni za Biden.

“Huu uchaguzi ujao ni muhimu katika ngazi zote kwa sababu tutapambana sio na mtu binafsi au chama bali changamoto kubwa. Kile tunapambana nacho ni mtindo mbaya wa ubinafsi, ukabila, mgawanyiko na kuona watu wengine kama maadui nchini Amerika,” Obama akaeleza.

Mmoja wa wasemaji wa Obama alidinda kusema lolote au kutoa ufafanuzi kuhusu kauli za kiongozi huyo.

Hata hivyo, Katibu wa Masuala ya Habari katika Ikulu ya White House Kayleigh McEnany Jumapili amepuuzilia mbali kauli za Obama kwenye taarifa aliyotoa kupitia shirika la habari la CNN.

“Hatua ambayo Rais Trump amechukua dhidi ya janga la corona ni ya kupigiwa mfano na imeokoa maisha ya Waamerika wengi.” akasema.

Kufikia sasa zaidi ya watu 67,000 wamefariki nchini Amerika kutokana na janga la corona huku wengine zaidi ya milioni moja wakipatikana na virusi hivyo.

Aprili 2020 Obama alitangaza wazi kwamba anaunga mkono azma ya Biden ya kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Democrat.

Na aliahidi kushiriki katika kampeni za mwanasiasa huyo mwenye umri mkubwa na aliye na tajriba pana katika sera za kigeni za Amerika.