COVID-19: Idadi ya Wakenya waliofariki ughaibuni yafika 20
Na CHARLES WASONGA
WIZARA ya Mashauri ya Kigeni imethibitisha kuwa jumla ya Wakenya 20 wamefariki kutokana na sababu zinazohusishwa na Covid-19.
Kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Jumapili, wizara hiyo ilisema kuwa Wakenya walipoteza maisha yao licha ya juhudi zilizochukuliwa kuwaokoa.
“Kati ya vifo hivyo 20, Wakenya 10 walifariki nchini Amerika, wanne wakafiriki nchini Uingereza, wawili nchini Italia huku Mkenya mmoja akifariki katika kila moja ya mataifa ya Uswisi, Saudi Arabia na Uswidi,” taarifa hiyo ikasema.
Wizara hiyo ilisema kuwa imekuwa ikiwasiliana na afisi za ubalozi wa Kenya katika mataifa ya kigeni kila mara tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotokea.
Takwimu za wizara hiyo zinasema kuwa zaidi ya Wakenya milioni tatu wanaishi ughaibuni, wengi wao wakiwa Amerika Kaskazini (400,000), Mashariki ya Kati (150,000), Asia na Australia (30,000) huku wengine wakiwa Magharibi mwa Uropa na Kusini mwa Afrika.
Wizara hiyo iliongeza kuwa Wakenya wengi walioko mataifa ya kigeni wamekuwa wakijaribu kusaka usaidizi kutoka kwa serikali kuhusiana na haja ya kurejea nyumbani.
“Wizara imekuwa ikiwasaidia wale waliokwama ng’ambo kufuatia kusitishwa kwa safari za kigeni katika mataifa hayo. Wale ambao wanaweza kujilipia nauli zao wataendelea kusaidiwa kurejea nchini,” taarifa hiyo ikasema.
Mnamo Jumapili asubuhi ndege ya Kenya Airways iliyokuwa imewabeba Wakenya 165 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutoka Guangzhou, China.
“Wengi wa waliorejea kutoka China ni Wakenya walioathirika na mlipuko wa virusi vya corona na kupoteza ajira. Wengine ni wanafunzi waliokamilisha masomo na wafanyabiashara waliozuiliwa huko kwa sababu ya changamoto za usafiri wa ndege.
Walipowasili nchini Wakenya hao walipelekwa katika vituo vya karantini walivyovichagua japo watakuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda wa wiki mbili.