• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
La Liga sasa kurejelewa Juni 12

La Liga sasa kurejelewa Juni 12

Na MASHIRIKA

RAIS wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Javier Tebas amefichua mipango ya kurejelewa kwa kampeni za kipute hicho msimu huu mnamo Juni 12.

Kwa mujibu wa kinara huyo, kwa sasa wanajitahidi kuhakikisha kwamba pana uwezekano wa “asilimia sufuri” wa mchezaji au afisa yeyote wa soka ya La Liga kupata virusi vya corona pindi kivumbi hicho kitakapoanza tena kwa pamoja na kile cha Daraja ya Kwanza (Segunda).

Vinara wa klabu zote 20 za La Liga walianza kuwapima wachezaji wao wiki jana huku mipangilio ya kurejelewa kwa mazoezi na mechi kusakatwa ndani ya viwanja vitupu bila mashabiki ikishika kasi.

“Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba tutakuwa tayari kuendeleza soka ya msimu huu kuanzia Juni 12,” akatanguliza Tebas katika mahojiano yake na kituo cha Movistar, Uhispania.

Hata hivyo, itatulazimu kuwa waangalifu zaidi kwa sababu kurejelewa kwa kampeni hizi kutategemezwa kwa mambo kadhaa ambayo hayahusiani moja kwa moja na soka, bali mienendo ya wanajamii,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba wachezaji wote watakuwa wakifanyiwa vipimo vya afya kila baada ya saa 24 kubaini iwapo wana virusi vya corona au la.

Tebas ameshikilia kwamba mechi za ligi nyinginezo za madaraja ya chini zitaanza kwa wakati mmoja (Juni 19) huku mechi za kitaifa zikiratibiwa kurejelewa Julai 31 ili kalenda ya soka ya Uhispania iwiane na ratiba ya Shirikisho la Soka Duniani na Shirikisho la Soka la Bara Ulaya ambalo limetaka fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kupigwa kufikia mwisho wa Agosti 2020.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, wachezaji watano wa soka ya Uhispania walipatikana na virusi vya corona licha ya kutoonyesha dalili zozote za kuugua ugonjwa huo kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya.

Kwa sasa wametengwa na watakuwa wakifanyiwa vipimo vya mara kwa mara hadi watakapothibitishwa kupona kisha waruhusiwe kuungana na wenzao katika kambi husika za mazoezi.

Viongozi wa La Liga walianza kuwapima wanasoka nchini Uhispania wiki jana, hii ikiwa sehemu ya mahitaji ya kimsingi yanayostahili kufanywa na klabu zote katika juhudi za kurejelewa kwa kampeni za soka msimu huu.

Uhispania ni miongoni ndilo la taifa la pili baada ya Italia katika bara Ulaya kuathiriwa zaidi na janga la corona baada ya maambukizi zaidi ya 264,000 kuripotiwa na takriban vifo 26,700 kutokea kufikia Mei 11, 2020.

You can share this post!

Klabu za EPL kurejesha mabilioni kwa wapeperushaji wa mechi...

ITABIDI MZOEE: Wakala afichua Ozil haondoki Arsenal hivi...

adminleo