• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Kuchezea Gor Mahia lilikuwa ni kosa kubwa, asema mvamizi wa City Stars

Kuchezea Gor Mahia lilikuwa ni kosa kubwa, asema mvamizi wa City Stars

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa Nairobi City Stars, Ezekiel Odera amesema kwamba anajutia maamuzi yake ya kusajiliwa na Gor Mahia mnamo 2011.

Ingawa chambo kilichotumiwa na Gor Mahia katika ofa ya kumshawishi kilikuwa kizuri zaidi wakati huo, Odera amesema heri asingemeza ndoano ya mabingwa hao mara 19 wa KPL na hivyo kusalia KCB ambapo aliwahi kufunga jumla ya mabao 10 katika msimu wake wa kwanza kwenye kipute cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

“Kutokana na udogo wa umri wangu wakati huo, nilikuwa na maazimio makubwa. Pia presha ilikuwa ya kiwango cha juu sana kwangu kipindi hicho. Iwapo ningalisalia kambini mwa KCB kwa mwaka mmoja zaidi, ingalikuwa vyema zaidi kwa taaluma yangu,” akasema.

Hata hivyo, Odera hajutii tukio la kukosa nafasi ya kusajiliwa na Ulinzi Stars wakati ambapo alikuwa amepoteza kitambulisho chake cha kitaifa na pia kutemwa kwenye kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki kipute cha Nile Basin nchini Misri baada ya kukosa kupata pasipoti.

“Kukosa kuingia katika sajili ya Ulinzi Stars na kutokuwa sehemu ya kikosi cha Stars wakati wa kivumbi cha Nile Tournament kulinifinyanga kwa namna mbalimbali,” akasema Odera aliyerejea katika kikosi cha City Stars muhula huu.

Kuhusu nafasi za kuvalia jezi za timu ya taifa ya Stars, Odera alisema: “Ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea timu ya taifa. Ni furaha yangu kwamba niliwahi kupata fursa ya kuwakilisha Kenya katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Uganda mnamo 2010 kisha kunogesha kipute cha Nile Basin mwanzoni mwa 2011,” akaongeza Odera ambaye kwa sasa amestaafu kwenye ulingo wa soka ya kimataifa.

Anakiri kwamba kipindi kilichowahi kumshuhudia akitamauka zaidi ni wakati ambapo usimamizi wa AFC Leopards ulimtuma kwa mkopo hadi kambini mwa KCB mnamo 2019 bila ya sababu yoyote hata ingawa wakati huo, ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Leopards ambao ni mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya KPL.

“Nilivunjika moyo, nikajisikitikia sana. Nilipitia wakati mgumu kwa hakika,” akasema.

Odera ambaye amecheza jumla ya mechi 177 za KPL na kupachika wavuni mabao 41 kwa sasa ana maazimio ya kuwa kocha wa kikosi chipukizi cha City Stars atakapoangika rasmi daluga zake za usogora.

Nyota huyo amewahi pia kuvalia jezi za Ushuru FC, Sofapaka na Thika United. Atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaokuwa kivutio cha mashabiki wa KPL msimu ujao baada ya kuwaongoza City Stars kupandishwa ngazi kutoka Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) msimu huu wa 2019-20.

You can share this post!

Lusaka atia muhuri kubanduliwa kwa Murkomen

CTWOO: Shirika lawafaa wengi kwa kusambaza chakula mitaa ya...

adminleo