Makala

AKILIMALI: Amekitegemea kilimo cha mboga na nyanya kimapato kwa miaka kadhaa

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na PHYLLIS MUSASIA

KIJIJI cha Kipsoni, Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu si tofauti na maeneo mengine nchini.

Wakazi wengi wa hapa wanajihusisha na kilimo cha mahindi, maharagwe na ufugaji.

Lakini kwake Elias Kiptoo, 28, amejaribu sana kuwa tofauti na wengine kwa kupanda mboga.

Shamba lake lina aina mbalimbali za mboga kama vile kabeji na managu huku sehemu kubwa ya shamba hilo ikiwa imejaa mimea ya nyanya.

“Nilianza ukulima mwaka wa 2015 pindi tu nilipokamilisha elimu ya sekondari kidato cha nne,” anasema Kiptoo.

Kiptoo anasema aliwaza jinsi ya kubadili hali na kujitafutia mapato kupitia kilimo na ndipo akaanza kulima.

“Kabla ya hapo, shamba hili lilikaa bure tu jinsi pia mimi mwenyewe nilivyokuwa sina kazi ya kufanya nyumbani,” anaeleza.

Anasema alianza shughuli nzima kwa takribani Sh60,000 ambapo kiasi kikubwa kilisimamia kilimo cha nyanya.

“Baada ya mavuno ya kwanza kuingia sokoni, kilimobiashara kilionekana kuwa kizuri na chenye manufaa. Na baada ya mwezi mmoja, nikawa ninauza mboga za takribani Sh7,000 kila wiki,” anasema.

Faida kutokana na mavuno, Kiptoo anasema alitumia kulima shamba mara tena na kuandaa sehemu ya upanzi uliofuata.

Elias Kiptoo (wa pili kushoto) akiwa shambani mwake katika kijiji cha Kipsoni, Moiben katika Kaunti ya Uasin Gishu. Ni mkulima wa mboga na nyanya na ameifanya kazi hiyo kwa miaka mitano sasa. Picha/ Stanley Kimuge

Wakati huu, Kiptoo analima shamba ekari 25 ambazo amekodi kwa miezi mitatu kwa ajili ya kilimo cha nyanya.

Kiptoo amemeweka mikakati kabambe kwa kuhakikisha kwamba nyanya hizo ziko katika viwango tofauti na anaweza kuvuna wakati tofauti.

“Nimefanya hivi ili kuhakikisha napata soko la bidhaa zangu wakati wote kwa mwaka mzima ili niwe na uwezo zaidi wa kifedha na pia kutayarisha shamba kwa upanzi mwingine kila wakati,” anabainisha.

Yeye ana uwezo wa kupanda mboga na nyanya mara tatu kwa mwaka lakini kwa sababu ya changamoto za soko, amechagua kupanda mara mbili tu.

Upanzi huu hufanyika kati ya Januari na Aprili na pia Agosti na Desemba wakati ambapo bei za bidhaa sokoni huwa nzuri kwa mkulima.

Kiptoo ametenga pia sehemu maalumu ambapo huandaa na kupanda mimea yake kabla ya kuisogeza shambani kwa upanzi rasmi baada ya wiki nne.

Yeye hutumia maji ya Mto Moiben pamoja na mbolea ya kujitengezea nyumbani na pia mbolea ya DAP kiasi kidogo.

“Baada ya mimea kutoka mchangani, huwa napalilia na kuinyunyuzia mbolea nyingine kabla ya kuongeza mchanga wa kutosha kwenye sehemu ya chini ya mizizi. Hii huipa mimea nguvu na uwezo wa kustahimili upepo na hata maji mengi,” anafafanua.

Ánaongeza kwamba, nyanya huchukua takribani siku 75 kukomaa na kuwa tayari kwa matumizi na soko.

Kutoka kwa shamba ekari moja, Kiptoo hupata kreti 400 za kilo 30 wakati kila kitu kimeenda sawa.

Huuza mazao yake katika masoko ya Moiben na Eldoret na wakati mwingine Nairobi na Uganda hasa msimu wa kiangazi.

Kreti ya kilo 60 huuzwa kwa Sh5,000 wakati bidhaa za nyanya huhitajika sana sokoni. Bei inaposhuka, Kiptoo huuza kiwango sawia kwa Sh3,000.

“Mapato ya mazao hutegemea nyakati. Kuna wakati ninaweza kupata Sh100, 000 na wakati mwingine ninapata Sh150,000 kwa kila ekari moja ya shamba,” akasema Kiptoo.

Hata hivyo, mkulima ana uwezo wa kupata hadi Sh500,000 wakati kilimo kimekubali na hali ni shwari.

Kiptoo anawasihi vijana wenzake kujitolea na kuwa wabunifu sio tu kwa kilimo ila kwa nyanja nyinginezo kama vile usanii, ufundi, na hata technolojia.

Anasema licha ya kuwa kupata nafasi za kazi humu nchini ina changamoto zake, hilo lisiwe jambo la kujitetea nalo.

Wakati huu kila mmoja anapaswa kujipanga na kujikakamua kwa lolote analofanya ili kupata riziki.

Kutokana na bidii yake, Kiptoo ameweza kujenga nyumba nadhifu na kujinunulia kipande cha shamba nusu ekari.

Hata hivyo, anapitia changamoto nyingi ikiwemo kupambanana na magonjwa na wadudu wanaoathiri mimea.

Nyanya ndizo huharibiwa zaidi na wadudu.

Mtaalamu wa kilimo na mimea Dkt Josia Chiveu wa Chuo Kikuu cha Eldoret anasema kilimo cha nyanya kinahitaji madini muhimu kama vile Potassium ili mkulima apate mazao ya kupigiwa mfano.

Madini haya kulingana na Dkt Chiveu husaida nyanya kuwa na ladha na pia harufu nzuri wakati wa mapishi.

“Mchanga ulio na kiwango cha juu cha asidi huchangia sana mimea ya nyanya kupoteza madini ya Potassium. Mkulima anapaswa kujaribu kupanda mimea tofauti kwenye shamba lake ili kuwa na usawa wa madini na viwango vya pH,” akasema Dkt Chiveu.

Anaonya kuhusu wakulima wanaomwagia mimea maji mengi kupita kiasi akisema kufanya hivyo kunatatiza mazao.