• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
COVID-19: Wakazi wengi wa Bonde la Ufa hawazingatii masharti ya kuzuia maambukizi

COVID-19: Wakazi wengi wa Bonde la Ufa hawazingatii masharti ya kuzuia maambukizi

BARNABAS BII na ONYANGO K’ONYANGO

WAKAZI wa eneo la Bonde la Ufa wamepuuzilia mbali masharti yaliyowekwa na serikali katika juhudi za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona na sasa wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.

Kwa sasa hoteli na maduka ya saluni, vinyozi, na kadhalika, yamefunguliwa kama kawaida.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika kaunti za Uasin Gishu, Trans-Nzoia, Elgeyo Marakwet na Nandi ulibaini kuwa baadhi ya biashara zimeondoa sabuni na maji ambayo wateja walitumia kunawa kabla ya kuhudumiwa.

Katika Kaunti ya Uasin Gishu, hoteli na maduka ya vyakula yanahudumu kama kawaida ilhali wahudumu hawajapimwa virusi vya corona kwa mujibu wa masharti ya Wizara ya Afya.

Wateja mjini Eldoret wanafurika hotelini bila kuketi umbali wa angalau mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine kama ilivyoagizwa na Wizara ya Afya.

“Tulifungua biashara zetu baada ya serikali kuruhusu hoteli zifunguliwe. Tusipofungua tutalisha nini watoto wetu?”akauliza mmoja wa wafanyabiashara wa mjini Eldoret aliyeomba jina lake libanwe kwa kuhofia kuandamwa na maafisa wa usalama.

Katika soko la Manispaa mjini Eldoret, wengi wa wafanyabiashara wanahudumia wateja wao bila kuvalia barakoa na hata kusongamana.

Wengi wa wanunuzi hawanawi mikono licha ya mapipa ya maji kuwekwa kwenye lango la soko hilo.

Mtu mmoja ameripotiwa kuwa na virusi vya corona katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Hongo

Maaskari wa kaunti wanadaiwa kuwatoza hongo ya Sh2,000 watu wanaopatikana hawajavalia barakoa.

Wanaokataa kutoa hongo hiyo wanapelekwa karantini kwa nguvu katika Shule ya Upili ya Kaplelach.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika vituo vya mabasi ulibaini kuwa wahudumu wa matatu sasa hawawapi sanitaiza abiria kabla ya kuingia ndani ya magari.

Misongamano imekuwa ikishuhudiwa katika vituo vya mabasi, maeneo ya kubugia chang’aa na supamaketi.

Gavana wa Uasin Gishu, Bw Jackson Mandago na Kamishna wa kaunti hiyo, Bw Abdirisack Jaldesa Jumatano walitoa onyo kali dhidi ya watengenezaji wa chang’aa.

Hali ni sawa na hiyo katika Kaunti ya Nandi ambapo watu wamekuwa wakitupa kiholela barakoa zilizotumika.

Waziri wa Afya wa Nandi Ruth Koech, Jumatano alionya kuwa wanaopatikana wakitupa ovyo maski zilizotumika watakamatwa na kushtakiwa kwa kuhatarisha maisha ya watu.

“Kadhalika, tumegundua kuwa baadhi ya watu wanabadilishana barakoa wanapotaka kuingia dukani. Hiyo ni hatari kwani virusi vinaweza kusambaa kwa urahisi kutoka mtu mmoja hadi mwingine,”akasema Bi Koech.

Hata hivyo, hali ni tofauti katika maeneo mbalimbali jijini Nairobi ambapo maduka makuu hayaruhusu mtu ambaye hajavalia barakoa kuingia ndani.

Katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi, hata hivyo, ni jambo la kawaida kukutana na misongamano ya watu; hali inayowaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.

You can share this post!

MTAISOMA NAMBA: Mo Farah aonya washindani wake mbio za mita...

Wakazi wa mitaa duni hawaamini virusi vinaweza kusambaa...

adminleo