Serikali ya kaunti ya Kiambu yapata mbinu ya kugawa chakula kwa walioathiriwa zaidi kiuchumi na janga la Covid-19
Na LAWRENCE ONGARO
KAUNTI ya Kiambu imeanza rasmi ugavi wa chakula walengwa wakiwa ni walioathiriwa zaidi na janga la Covid-19 ambalo limelazimu shughuli nyingi za uzalishaji kiuchumi kukwama.
Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema tayari wamepata majina ya watu wote wanaostahili kupokea msaada huo, na wako tayari kuendesha shughuli hiyo.
“Tunawapongeza wahisani wote waliojitolea kwa hali na mali kusaidia waathiriwa wote wanaopitia hali ngumu katika kaunti hii. Shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia ya uwazi bila ubaguzi wowote,” alisema Dkt Nyoro.
Alisema awamu ya kwanza italenga familia zipatazo 8,500 katika kaunti ya Kiambu ambapo itafanyika kwa utaratibu unaostahili.
Alisema kulingana na mpangilio wao, watasambaza unga wa ugali kilo 17,000, unga wa chapati kilo 18,500, mcheli kilo 17,000, na mafuta ya kupikia lita 17,000.
Alizipongeza kampuni 19 ambazo zimejitolea kuona ya kwamba zinakabiliana na janga la Covid-19 kwa kutoa misaada hiyo.
“Tunapongeza juhudi za kampuni na mashirika mbalimbali kujitolea mhanga kuona ya kwamba wakazi wa Kiambu wanapokea msaada wakati huu homa kali ya corona ikizidi kuyumbisha maisha ya kawaida ya raia,” alisema Nyoro.
Alisema chakula hicho kitasambazwa kupitia kamati maalum iliyoteuliwa hivi majuzi kwa ushirikiano na machifu wa mashinani.
Alisema tayari Kaunti ya Kiambu imepokea mchele kilo 2,000 kutoka kwa Wizara ya Ugatuzi ili kusaidia walioathirika na njaa kutokana na athari za Covid-19.