Makala

BURUDANI: Akeelah aahidi kuzingatia ushauri wa produsa talanta ifike kilele

May 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MSANII chipukizi Fatma Hemedi Yahyah almaarufu Akeelah ni miongoni mwa kina dada waliobahatika katika ukanda wa Pwani kuwa na uhuru wa kuchagua wanayotaka kuyatekeleza katika maisha yao, kupitia vipaji vyao.

Ni wazazi wachache Pwani ya Kenya wenye kuwapa mabinti zao uhuru wa kujichagulia yale wanayotaka kuyatekeleza ambayo wanafikiria ndiyo yatakayowanufaisha katika maisha yao.

Akeelah alibahatika kupewa na mama yake uhuru wa kuchagua alilotaka kutekeleza kwa manufaa ya maisha yake ya baadaye.

“Sikuwahi kupata malezi ya babangu sababu yeye na mama waliachana nikiwa na umri wa mwaka mmoja na hivyo nilipoinukia na kifo cha babangu kilipotokea nikiwa na umri wa miaka 15, uteuzi wangu ukawa ni sanaa ya muziki,” anasema Akeelah.

Chipukizi Akeelah anasema alichukua uamuzi wa kuwa mwanamuziki kwa sababu alitambua ana talanta katika fani hiyo na kutegemea kuwa ndiyo itaweza kumfanikisha maishani.

Kwa kuanzia, Akeelah alifanya cover mbili; ‘Naenjoy’ ya Aslay na ‘Ate’ ya Mbosso.

Kuthibitisha msanii huyo ameanza kwa kishindo ni kuwa wimbo ‘Naenjoy’ alioutoa kipindi cha miezi mitatu iliyopita umesikizwa na wapenzi wa muziki zaidi ya 125,000 kupitia kwa YouTube.

Fatma Hemedi Yahyah ‘Akeelah’. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Kibao hicho kingine cha ‘Ate’ kimevutia zaidi ya mashabiki 76,000.

“Kiuhakika, sina budi kuwashukuru wapendao muziki kwa kuniunga mkono na kunifanya nipate motisha zaidi wa safari niliyoanza ya kufanikiwa kwa lengo langu la kuwa mwanamuziki wa kutambulika,” anasema.

Akeelah alishirikishwa na msanii anayeinukia kwa kasi Ally Mahaba kwenye wimbo ‘Ujitume’ uliozinduliwa miezi miwili iliyopita na hadi sasa kusikilizwa na wapendao muziki wanaozidi 319,000.

Kibao chake cha kwanza alichoimba peke yake na kukizindua Machi 22, 2020, ni kile cha ‘Nikuache’ na kwa muda mfupi, tayari kimesikizwa na mashabiki 104,000.

Kutokana na tarakimu za nyimbo alizowahi kuimba zikiwemo na za cover, Akeelah ameanza kutambulika kuwa ni miongoni mwa wasanii maarufu wa Pwani.

“Kufanikiwa kwangu kunatokana na produsa na mwalimu wangu Awadh Salim Awadh almaarufu Shirko ambaye anaendelea kunifunza jinsi ya kuweza kupanda ngazi na kuwa mwimbaji mwenye kipaji sawa na waimbaji wenye majina makubwa,” anaeleza.

Akeelah anasema hamu yake kubwa ni kufanya kolabo na waimbaji mashuhuri wakiwemo Masauti, Nadia Mukami, H_Art the Band na Sanaipei (Wakenya), Mbosso, Aslay, Nandy na Marioo (Watanzania).

“Natambua nikiimba nao na kwa kuwa wanatambulika kote Afrika Mashariki, umaarufu wangu utapanda kwa kasi. Namwachia produsa wangu Shirko anipangie mipango ya kufanya kolabo nao kwani baadhi yao yeye ndiye kawainua,” anaweka wazi.

Kwa wakati huu, Akeelah anaendelea kutayarisha vibao kemkem ambavyo ana uhakika mashabiki wake watavipenda.

“Kutokana na sapoti waliyonipa mashabiki wangu hasa kwa wimbo wangu wa kwanza wa ‘Ujitume’, nina hakika watazipenda zaidi nitakazozitoa,” anasema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 20 anasema ana matarajio makubwa ya kufikia lengo lake la kuwa mwimbaji wa kimataifa hasa kwa kuwa ameona dalili nzuri kutokana na wafuasi wengi kuusikiliza wimbo wake huo wa ‘Ujitume’.

Fatma Hemedi Yahyah ‘Akeelah’ akiwa ameshika maikrofoni. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Akeelah anasema ana hamu pia ya kufanya safari kutembelea nchi jirani za Tanzania na Uganda kwa ajili ya kushuhudia waimbaji mahiri wa mataifa hayo.

“Nina imani nitasoma mambo fulani ambayo nitayaiga katika safari yangu ya mafanikio kimuziki,” akasema.

Produsa Shirko anasema mbali na kipaji alichonacho Akeelah, ana matumaini makubwa ya kuweza kuwa mwimbaji maarufu barani Afrika na kuwa miongoni mwa waimbaji wachache wa kike waliopata heshima na tuzo kubwa kwa kuzitangaza vyema nchi zao kwa mataifa ya ng’ambo.

“Akeelah angali anahitaji mafunzo ya ziada aielewe sanaa ya muziki kiujumla kwani bado ni mdogo kwenye tasnia hiyo. Pia namshauri aepukane na vishawishi awasikilize waliomtangulia kiumri na maarifa ili afanikiwe kwa mahitaji yake,” akasema Shirko.