Waiguru alalama wapinzani wake wanamhujumu
WANDERI KAMAU na GEORGE MUNENE
GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga, amejitetea vikali kuhusu utendakazi wake, akiwalaumu mahasimu na washindani wake katika Chama cha Jubilee (JP) kwa masaibu yanayomkumba.
Mnamo Jumatano, mamia ya wakazi katika kaunti hiyo walifanya maandamano katika mji wa Ngurubani wakishinikiza gavana huyo kung’olewa mamlakani.
Wakazi hao walimlaumu kwa kujikokota kutekeleza miradi ya maendeleo na kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi.
Lakini kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Alhamisi, gavana huyo alihusisha masaibu yake na “watu wenye ushawishi” katika chama hicho, aliodai wanampiga vita kwa kumtumia Naibu Gavana Peter Ndambiri na madiwani katika Bunge la Kaunti ya Kirinyaga.
“Kuna watu katika Jubilee ambao wamekuwa wakimtumia naibu wangu na madiwani kunipiga vita kisiasa kutokana na rekodi yangu nzuri ya maendeleo. Sina hofu hata kidogo. Niko tayari kuwakabili,” akasema.
Uhasama
Kumekuwa na tofauti kali kati ya gavana na naibu wake, akisema anaendesha njama za kichinichini kumwondoa mamlakani, akilenga kuwania nafasi hiyo mnamo 2022.
Gavana pia amekuwa akiwalaumu Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho na Mwakilishi wa Wanawake, Bi Wangui Ngirici, kuwa miongoni mwa watu “wanaoingilia” utendakazi wake.
Kwenye maandamano hayo, wakazi walimlaumu gavana kwa kuchelewesha mishahara ya wahudumu wa afya.
Wakazi hao wenye ghadhabu waliacha shughuli zao za kawaida katika mji wa Ngurubani, ili kushiriki maandamano hayo.
Hali ya taharuki ilitanda katika eneo hilo, kwani baadhi yao waliwazuia waendeshaji magari kuendelea na safari zao huku wengine wakiwahangaisha.
Wakiwa wamebeba mabango, waliilaumu serikali ya Bi Waiguru kwa kukosa kuimarisha hali ya barabara na kutowalipa wafanyakazi mishahara yao.
“Lazima Waiguru aende! Lazima Waiguru aende!” akasema mmoja wa wakazi.
Wakiongozwa na Bw Michael Chomba, walimlaumu gavana kwa kutoshughulikia malalamishi ya wafanyakazi, huku wakilitaka Bunge la Kaunti kumng’oa mamlakani.
“Barabara ziko katika hali mbaya huku wahudumu wa afya wakiwa hawajalipwa mishahara kwa miezi miwili. Serikali hii pia haishughulikii masaibu ya watu walioathiriwa na mafuriko katika kijiji cha Githogondo kati ya maeneo mengine,” akasema.
Hata hivyo, Bi Waiguru alisema ucheleweshaji huo ulichangiwa na “matatizo kadhaa” yaliyotokea kwenye Hazina Kuu ya Serikali.
“Binafsi, mshahara wangu ulichelewa kwa miezi miwili. Lazima wafanyakazi waelewe wakati mwingine matatizo haya hutokea. Hata hivyo, hawawezi kunyimwa mishahara yao hata ichelewe kwa kwa muda upi,” akasema.
Wakati huo huo, imebainika kwamba huenda madiwani 11 walioshiriki kwenye mchakato wa jaribio la kumng’oa mamlakani Bi Waiguru wakafukuzwa katika Jubilee.
Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho katika kaunti hiyo, Bw Muriithi Kang’ara, huenda madiwani wakachukuliwa hatua kama walivyofanyiwa aliyekuwa Kiongozi wa Wengi kwenye Seneti, Bw Kipchumba Murkomen na aliyekuwa Kiranja wa Wengi, Bi Susan Kihika.