• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Afueni adimu kufuatia mafuta kushuka bei

Afueni adimu kufuatia mafuta kushuka bei

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA wanatarajia sasa kupata afueni baada ya Mamlaka ya Kawi na Petroli (EPRA) kupunguza bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa.

Bei ya petroli imepungua kwa Sh9.54 huku dizeli ikipungua kwa Sh19.19 kwa kila lita. Hiyo inamaanisha kuwa kuanzia Ijumaa wenye magari jijini Nairobi watanunua mafuta ya petroli kwa Sh83.33 kwa kila lita.

Wateja wa dizeli pia wamepata afueni kwani sasa watanunua mafuta kwa Sh78.37 kwa kila lita.

Jijini Mombasa, lita moja ya petroli itauzwa kwa Sh80.85, dizeli Sh75.88 na mafuta ya taa Sh77.29

Bei mpya ya mafuta ya petroli mjini Eldoret ni Sh84.20, dizeli Sh79.38 na mafuta ya taa Sh80.78

Mjini Kisumu, mafuta ya petroli yatauzwa kwa Sh84.19, dizeli Sh79.37 na mafuta ya taa Sh80.77 hadi Juni 14 ambapo mamlaka ya EPRA itatangaza bei mpya.

Katika miji ya Lokitaung na Lokichogio, Kaunti ya Turkana mafuta ya petroli yatauzwa kwa Sh92.02 na Sh91.16 mtawalia.

Mafuta ya petroli yamekuwa yakiuzwa kwa Sh92.87 kwa kila lita tangu Aprili 15, huku kiasi sawa cha dizeli kikiuzwa kwa Sh97.56

Tangu Machi, mwaka huu bei ya mafuta imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa hivyo kutoa afueni kwa Wakenya ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi iliyosababishwa na janga la virusi vya corona.

Wamiliki wa matatu, hasa jijini Nairobi, wamekuwa wakishutumiwa kwa kuwatoza abiria nauli ya juu licha ya bei ya mafuta kupungua.

Bei ya mafuta imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya serikali kutupilia mbali ombi la wafanyabiashara wa mafuta waliotaka serikali isipunguze bei kwanza kutoa nafasi kwao kuuza mafuta ghali waliyonunua Aprili.

Bei hiyo mpya inamaanisha kuwa wauzaji wa petroli watalazimika kuuza mafuta waliyosalia nayo kwa bei mpya.

Katibu wa Wizara ya Kawi na Petroli, Bw Andrew Kamau alikataa ombi la wafanyabiashara hao huku akisema kuwa punguzo hilo linaongozwa na sheria na wala si shinikizo kutoka kwa wafanyabiashara.

You can share this post!

Vijana wazua fujo kudai malipo ya Mpango wa Usafi wa mitaa

Mwanamume azuiliwa kujeruhi polisi kwa jiwe wakati wa kafyu

adminleo