Kimataifa

RWANDA: Mshukiwa wa mauaji ya halaiki ya 1994 Felicien Kabuga akamatwa nchini Ufaransa

May 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

MUUNGANO wa walionusurika na wahasiriwa wa mauaji ya halaiki nchini Rwanda mnamo 1994 dhidi ya kabila la Watutsi Jumamosi wamefurahia habari za kukamatwa kwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Felicien Kabuga.

Kabuga alikamatwa mapema jijini Paris, Ufaransa na maafisa wa serikali ya nchi hiyo ya bara Uropa.

Alihukumiwa na Mahakama ya Kitaifa ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uhalifu Rwanda (ICTR) mnamo 1997 kwa makosa saba, yakiwemo mauaji ya halaiki, kupanga mauaji hayo, na kuchochea utekelezaji wa mauaji hayo.

“Tunafurahia habari za kukamatwa kwa Kabuga ambaye amekuwa akisakwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa mauaji ya halaiki dhidi ya Tutsi mnamo 1994. Hizi ni habari njema,” Jean-Pierre Dusingizemungu aliambia runinga ya Rwanda.

Dusingizemungu ndiye Rais wa IBUKA, ambao ni muungano wa walionusurika na wahasiriwa wa mauaji hayo ya halaiki nchini Rwanda.

“Hii ni afueni kubwa kwetu wakati huu tukiendelea na ukumbusho wa Mauaji ya Halaiki dhidi ya Watutsi,” akaeleza.

Rwanda huandaa hafla ya ukumbusho wa mauaji hayo kuanzia Aprili 7 hadi Julai 4 kila mwaka, muda ambao unashabihiana na kipindi cha siku 100 ambapo mauaji hayo yalitekelezwa.

Kuna washukiwa wengine wa mauaji hayo ambao bado wamejificha katika mataifa ya kigeni.

Dusingizemungu ametoa wito kwa mataifa ambayo bado yamewapa hifadhi yawakamate na kuwawasilisha mahakamani waadhibiwe.

Kabuga alikamatwa kutokana na uchunguzi ulioendeshwa kwa pamoja na serikali hiyo na Afisi ya Kiongozi wa Mashtaka katika Jopo la Kimataifa kuhusu Uhalifu (IRMCT).

Afisi ya kiongozi wa mashtaka ya umma nchini Rwanda hufanya kazi kwa ushirikiano na jopo la IRMCT kuwasaka na kuwakamata washukiwa wa mauaji hayo ya halaiki.

“Kabuga amekamatwa kutokana na ushirikiano wetu na asasi husika za kimataifa kama vile jopo la IRMCT,” amesema Faustin Nkusi ambaye ni msemaji wa Mamlaka ya Mashtaka ya Umma Rwanda.